Dar es Salaam. Kwa upande fulani tunaweza kusema muziki wa Bongo Fleva umepata bahati ya kuwapokea wanasoka maarufu duniani, Lionel Messi na Mesut Ozil ukiwa ni mwaliko kutokana na kuzikonga nyoyo za mashabiki wao nchini.

Wawili hao wamepokelewa na mastaa wa Bongo Fleva, Stamina na Madee ambao wamewakaribisha hadi majumbani kwao na wanaishi nao katika famili zao kwa miaka sasa.

Je, ni lini hasa Messi na Ozil walikuja nchini na kutinga kwenye Bongo Fleva?, na walifikaje kwenye familia za Stamina na Madee hadi kuanza kuishi nao?

Stamina kutokea kundi la Rostam, Desemba 2020 alijaliwa kupata mtoto wa kiume na kumpa jina la Lionel kama heshima kwa mcheza soka kutokea Argentina, Lionel Messi.

Rapa huyo alieleza ameamua kumpa mwanae jina la Lionel kwa sababu ya ushabiki wake kwa FC Barcelona na mapenzi aliyonayo kwenye soka, na mchezaji wake bora, Messi.

Ikumbukwe Messi anayekipiga Inter Miami ya Marekani kwa sasa, aliichezea Barcelona kwa miaka 21, akicheza mechi 778 na kufunga magoli 672 tangu ajiunge nayo akiwa na umri wa miaka 13.

Kwa upande wake Madee kutokea Tip Top Connection na Manzese Music Baby (MMB), katikati ya Decemba 2020, alitangaza kupata mtoto wa kwanza wa kiume na mpenzi wake, Mina.

Kama alivyofanya Stamina, Madee naye aliamua kumpa mtoto wake jina la Ozil kama kuonyesha mapenzi yake kwa mchezaji Mesut Ozil ambaye wakati huo bado alikuwa anaichezea Arsenal ambayo ni klabu anayoishabikia ndani ya EPL.

Ozil ni mtoto wa tatu kwa Madee baada ya Saida na Chonge ambaye amekuwa maarufu mtandaoni huku akitokea kwenye video kadhaa za muziki kama Funga Geti ya Billnass na Hadidhi 2060 ya Madee.

Ikumbukwe Mesut Ozil aliyekuwa akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, alijiunga na Arsenal mwaka 2013 akitokea Real Madrid kwa dau la Pauni42.4 milioni.

Katika safari yake ya soka alifanikiwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ujerumani mara tano, huku akilisaidia taifa lake kutwaa Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil kabla kustaafu timu ya taifa mnamo 2018.

BONGO FLEVA NA SOKA

Ukiachilia mbali uwezo wake mkubwa katika muziki, mwimbaji wa Bongo Fleva, Ruby alikuwa mchezaji soka mzuri tu akicheza namba nane uwanjani wakati huo alikuwa akiichezea Young Twiga Stars.

Baada ya kuitumika timu hiyo, kipaji chake kingine kilionekana na Tanzania House of Talent (THT) na alikutana na Barnaba ambaye alimwandikia wimbo wake ‘Na Yule’ uliomtoa kimuziki.

Kufanya vizuri kwa wimbo huo kukamtenga mbali na soka lakini anasema kama angetia juhudi upande huo leo anagekuwa na simulizi nzuri zaidi.

Alikiba, mwanzilishi wa Kings Music aliyetoka na albamu yake, Cinderella (2007), wengi wanamfahamu kama mchezaji mzuri wa mpira na amewahi kuzichezea timu za wasanii katika mabonanza mbalimbali.

Alikiba ambaye ni shabiki wa Liverpool FC, sio mgeni katika soka na matukio yake, ndiye staa mkubwa wa kwanza wa Bongo Fleva kucheza Ligi Kuu Bara baada ya kusajiliwa na Coastal Union msimu wa 2018/2019.

Utakumbuka mnamo Oktoba 2023, Alikiba alitumbuiza katika ufunguzi wa mashindano ya African Football League (AFL) uliofanyika Uwanja wa Mikapa, Dar es Salaam kwa kukaribisha pambano kati ya Simba SC dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Alikiba ndiye msanii pekee wa Bongo Fleva aliyechaguliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutumbuiza katika mashindano hayo ambayo ndio ilikuwa mara ya kwanza yanafanyika kwa kushirikisha klabu nane za Afrika, na hadi sasa hajafanyika tena.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *