Dar/Songwe. Wakulima wa ufuta nchini wana matarajio makubwa kufuatia uzinduzi wa biashara ya ufuta katika msimu wa 2026/27 unaoanza kufanyika leo Ijumaa, Mei 8, 2026, mkoani Songwe.
Serikali na wadau wamesisitiza kuimarishwa kwa ubora wa zao hilo katika soko ambalo ushindani wake umeendelea kuongezeka katika medani ya kimataifa.
Hata hivyo, matarajio hayo yanajikita katika ongezeko la uzalishaji ikilinganishwa na msimu uliopita, kufuatia juhudi mbalimbali za serikali kupitia taasisi mbalimbali, ikiwamo Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mengine (COPRA).
Matarajio hayo yanaenda sambasamba na matarajio ya kuimarika kwa bei, ingawa mazingira ya soko la kimataifa yanaendelea kuamuliwa kwa kiasi kikubwa na nguvu ya soko hasa mahitaji na upatikanaji wa bidhaa husika.
Pia, biashara hiyo inaongozwa na mabadiliko ya mahitaji nchini China, ushindani kutoka kwa wazalishaji wapya, pamoja na kupanda kwa gharama za usafirishaji, hivyo kuathiri moja kwa moja mapato ya maelfu ya wakulima wadogo nchini.
Ingawa Tanzania imeendelea kujipambanua kama mmoja wa wasambazaji wakuu wa ufuta wenye ubora barani Afrika, sekta hiyo inafanya kazi katika mazingira ambayo bei za bidhaa huamuliwa zaidi nje ya mipaka ya nchi.
Hali hii huifanya Tanzania na wazalishaji wengine wa Afrika kuwa na ushawishi mdogo katika kupanga bei za kimataifa, licha ya mchango wao mkubwa katika usambazaji wa bidhaa hiyo.
Soko la kimataifa la ufuta
Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa biashara ya ufuta duniani inategemea kundi dogo la wanunuzi wakubwa, huku Asia ikiwa kitovu kikuu cha mahitaji.
China inaendelea kuwa mnunuzi mkubwa zaidi, ikiagiza kati ya tani 900,000 hadi milioni 1.1 kila mwaka kwa ajili ya kukamua mafuta, usindikaji wa vyakula, utengenezaji wa peremende na akiba ya kimkakati.
Japani huagiza kati ya tani 150,000 hadi 170,000, hasa ufuta wa ubora wa juu unaotumika katika vyakula vya moja kwa moja na bidhaa za kukaangwa.
Uturuki huagiza kati ya tani 140,000 hadi 160,000 kwa ajili ya uzalishaji wa tahini na halva, wakati India huingiza kati ya tani 100,000 hadi 130,000, ambazo nyingi husafishwa na kusafirishwa tena kwenye masoko yenye thamani kubwa.
Korea Kusini huagiza kati ya tani 70,000 hadi 90,000 kupitia zabuni, wakati Israel hutumia kati ya tani 50,000 hadi 65,000.
Marekani huagiza takriban tani 45,000 hadi 55,000 kwa ajili ya viwanda vya mikate na vyakula vilivyosindikwa, huku Vietnam ikiongeza kasi ya matumizi yake hadi kati ya tani 35,000 na 50,000 kila mwaka kutokana na ukuaji wa sekta ya chakula.
Kwa upande wa uzalishaji, Sudan inaongoza duniani kwa kuzalisha wastani wa tani milioni 1.25 mwaka 2025, ikifuatiwa na India (tani 850,000), Brazil (tani 400,000) na Ethiopia (tani 380,000).
Tanzania licha ya uzalishaji mdogo, bado ina nafasi muhimu kutokana na ubora wa ufuta unaozalishwa na sifa nyingine za ubora wa mbegu zake.
Wachambuzi wa masuala ya kilimo wanasema muundo huo umejenga mfumo wa bei unaotawaliwa na wanunuzi, kwa sababu wazalishaji wa Afrika wana nafasi ndogo ya kuathiri bei licha ya kuwa msingi wa usambazaji wa bidhaa hiyo.
Mabadiliko ya uzalishaji Tanzania
Uzalishaji wa ufuta nchini umekuwa ukibadilika kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kutokana na changamoto mbalimbali, takwimu zinaonyesha uzalishaji ulipungua kutoka tani 236,162 mwaka 2020/21 hadi tani 79,170 mwaka 2021/22.
Hata hivyo, uliongezeka hadi kufikia tani 266,994 mwaka 2022/23 kabla ya kushuka tena na kusimama karibu tani 240,010 mwaka 2023/24.
Mwaka 2024/25, uzalishaji ulifikia tani 257,040, hali inayoashiria kuimarika kwa kiasi fulani.
Kwa msimu wa 2026/27, serikali inatarajia ongezeko zaidi kutokana na mipango iliyofanywa ikiwemo kusambaza mbegu bora na pembejeo kwa wakulima.
Hata hivyo, wataalamu wa kilimo wanaonya kuwa uthabiti wa uzalishaji bado ni dhaifu kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mvua zisizotabirika, gharama kubwa za pembejeo na uchakavu wa udongo katika baadhi ya maeneo.
Mikoa inayoongoza
Mkoa wa Lindi unaendelea kuongoza uzalishaji wa ufuta nchini, ukichangia tani 75,759 zenye thamani ya Sh221.5 bilioni mwaka 2025.
Mikoa mingine inayoongoza ni Pwani yenye tani 27,381 (Sh75.2 bilioni), Morogoro tani 26,055 (Sh66.9 bilioni), Mtwara tani 22,697 (Sh64.2 bilioni) na Dodoma tani 20,565 (Sh56.2 bilioni).
Kwa ujumla, thamani ya uzalishaji wa ufuta nchini ilifikia takriban Sh595.6 bilioni, hatua inayothibitisha mchango mkubwa wa zao hilo katika pato la taifa na biashara ya nje, sambamba na mazao kama korosho na kahawa.
Mabadiliko ya bei sokoni
Licha ya kuongezeka kwa uzalishaji, mwenendo wa bei umekuwa changamoto kwa wakulima.
Mwaka 2023/24, wastani wa bei ulikuwa Sh3,000 kwa kilo, ukaongezeka kidogo hadi Sh3,144 mwaka 2024/25 kabla ya kushuka hadi Sh2,329 mwaka 2025/26.
Makadirio ya msimu wa 2026/27 yanaonyesha uwezekano wa bei kubaki imara lakini chini ya shinikizo la soko la kimataifa.
Wachumi wa kilimo wanahusisha kushuka kwa bei na ongezeko la uzalishaji duniani, ushindani kutoka kwa nchi kama Brazil na Sudan, pamoja na kupungua kwa kasi ya ununuzi nchini China.
“Mfumo wa soko la ufuta sasa unaendeshwa na ushindani zaidi kuliko uhaba. Nchi inapoongeza uzalishaji, bei hubadilika haraka,” alisema mtaalamu mmoja wa masoko ya kilimo kwa sharti la kutotajwa jina.
Gharama za usafirishaji
Gharama za usafirishaji zimeendelea kuwa changamoto nyingine kubwa. Kutokana na misukosuko ya kisiasa na kiusalama katika Bahari ya Shamu na Mashariki ya Kati, ada za bima na usafirishaji zimepanda kwa kasi.
Mimea ya ufuta ikiwa shambani. Picha na Maktaba
Wasafirishaji wanasema gharama hizo zimeongezeka kwa viwango vya tarakimu mbili katika baadhi ya njia, hususan kupitia vituo vya Dubai vinavyotumika kusafirisha ufuta kwenda Asia na Ulaya.
“Kipengele cha usafirishaji sasa ni sehemu kubwa ya bei ya mwisho. Hata kama mahitaji yako imara, gharama za usafiri zinapunguza faida ya mkulima,” aliongeza mtaalamu huyo.
Nafasi ya China
China inaendelea kuwa mhimili mkuu wa soko la ufuta duniani. Sio tu kwamba ni mnunuzi mkubwa, bali pia huathiri mwenendo wa bei kimataifa.
Tanzania husafirisha China aina mbili kuu za ufuta: ghafi wa mafuta na ule wa ubora wa juu kwa matumizi ya chakula.
Wachambuzi wanasema muundo wa mahitaji wa China unaiwezesha kushawishi bei katika sehemu zote za soko la chini na la juu.
Hata hivyo, kuongezeka kwa ushindani kutoka Brazil kunabadilisha mwelekeo wa biashara.
“Brazil inanufaika na uzalishaji wa kisasa na gharama ndogo, jambo linaloanza kupunguza faida ya bei kwa wazalishaji wa Afrika,” alisema mtaalamu huyo.
Pamoja na hayo, Tanzania bado ina nafasi kutokana na ubora mkubwa wa ufuta wake unaopelekea kupatikana kwa kiwango kikubwa cha mafuta, mara nyingi zaidi ya asilimia 50, jambo linaloufanya kuvutia masoko mbalimbali duniani hasa Japan na Ulaya.
Uongezaji thamani
Wataalamu wanashauri Tanzania kuwekeza zaidi katika uongezaji thamani badala ya kuuza malighafi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Lutengano Mwinuka, anasema kuuza ufuta ghafi kunaifanya nchi kuathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya bei za kimataifa.
“Bila kuwekeza katika mafuta, rojo au bidhaa za chakula zilizosindikwa, Tanzania itaendelea kuwa mpokeaji wa bei tu,” alisema.
Kauli ya wakulima
Mkulima wa ufuta kutoka kijiji cha Chang’ombe, kata ya Chang’ombe wilayani Songwe, Vicent Msawila amesema mauzo ya zao hilo kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani yamewanufaisha wakulima tofauti na awali walipouza kwa walanguzi ndoo moja Sh2,000.
Msawila amesema kati ya 2022 hadi 2024 wakulima walipata bei kati ya Sh3,000 na Sh4,000 kwa kilo hali iliyowavutia wengi kuingia kwenye kulima ufuta na kuongeza uzalishaji.
Hata hivyo, alisema msimu uliopita kulikuwa na changamoto ya bei ambapo ufuta uliuzwa wastani wa Sh2,400 kutokana na changamoto mbalimbali.
“Jambo hilo liliwafanya wakulima waliokopa kwenye taasisi za kifedha kushindwa kurejesha mikopo yao,” amesema Msawila.
Ameiomba serikali kupunguza tozo zinazochangia kupanda kwa bei, akisema wanunuzi hujumuisha tozo zote kabla ya kuweka bei ya mwisho inayolipwa mkulima.
“Awali mfumo wa stakabadhi ghalani ulionekana kutowanufaisha wakulima, lakini sasa umewasaidia kupata masoko yenye tija na kuuza ufuta kwa bei nzuri tofauti na awali walipouza kwa hasara,” alisema.
Mkazi wa kijiji cha Mgamba kata ya Magamba wilayani humo, Amina Sikazwe amesema wakulima wananufaika kupitia vyama vya ushirika ambapo makampuni hutangaza bei na anayetoa bei ya juu hukubalika, na bei ikishuka mnada husitishwa na kurudiwa.
“Mei 8–9, 2026 tunatarajia kuzindua mnada wa ufuta mkoani Songwe. Matarajio ni kupata bei nzuri walau kufikia Sh4,000 kwa kilo, hivyo kuwanufaisha wakulima,” alisema Sikazwe.
Sikazwe amesema wananchi hutumia kipato cha ufuta kujenga nyumba, kulipia elimu ya watoto wao na kuendeleza shughuli za ujasiriamali.
Mkazi mwingine, Paulo Sinkala, amesema uzalishaji unatarajiwa kuongezeka kutokana na uungwaji mkono wa serikali hususan huduma za ugani.
Amesema ardhi imeanza kuchoka hali inayoshusha uzalishaji na kuitaka Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kuongeza kasi katika utekelezaji wa mpango wa kuongeza tija.
“Tunaomba COPRA waongeze juhudi za utafiti ili walete mbegu bora na pembejeo zingine ili kuongeza uzalishaji kwani tumekuwa tukilima kwa mazoea,” alisema, akishukuru kwa hatua zilizoanza kuchukuliwa.
Mkulima Fedson Njela amesema kuelekea mnada wanahofia kushuka kwa bei ikilinganishwa na mwaka jana walipouza kwa Sh2,400 kwa kilo.
“Gharama za uzalishaji ni kubwa zikiwemo kukodi mashamba, kupalilia, kupiga dawa na kusafisha ambapo ekari moja hupata wastani wa gunia mbili na nusu ambazo hazitoshi kufidia gharama walizotumia,” amesema.
Aidha, wakulima hao wamesema wanaendelea kushirikiana na vyama vya ushirika ili kuhakikisha wanapata taarifa sahihi za bei, masoko na muda wa mnada, hatua inayosaidia kupunguza utegemezi kwa walanguzi na kuongeza uwazi katika biashara ya ufuta katika maeneo yao ya uzalishaji wilayani Songwe.
Wameeleza kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani umeongeza ushindani wa soko, kuwapa nafasi wakulima wadogo kushiriki mauzo ya pamoja na kuboresha kipato chao kwa ujumla, jambo linalochochea maendeleo ya kilimo cha ufuta katika maeneo ya vijijini mkoani Songwe na kuinua uchumi wa kaya zao wilayani Songwe.
WRRB na maandalizi ya msimu
Mkurugenzi Mtendaji wa COPRA Irene Madeje Mlola alisema maandalizi ya msimu mpya yamekamilika.
“Miongozo inabaki ile ile ya mwaka jana, isipokuwa tumerekebisha kidogo tozo za usafirishaji kutokana na hali ya kimataifa,” alisema.
Aliongeza kuwa mfumo wa usimamizi umeimarishwa kwa ushirikiano wa maafisa wa serikali za mitaa na vyama vya ushirika, huku wanunuzi wakipewa fursa ya kukagua bidhaa iliyoko ghalani kabla ya mnada.
“Uwazi umeongezeka kupitia mfumo wa video na ukaguzi, ili kuhakikisha ubora wa bidhaa unalingana na taarifa zilizotangazwa,” alisema.
Chama cha Ushirika Songwe
Akizungumza wakati wa jukwaa la wadau wa sekta ya ufuta sambamba na ufunguzi wa msimu wa ufuta, mkurugenzi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Songwe (Sorecu), Daudi Andrew Slahhi, alisema katika msimu wa 2026/2027, ushirika umechukua hatua mbalimbali kushughulikia changamoto zilizojitokeza msimu uliopita, pamoja na kuendelea kuboresha huduma kwa wakulima na vyama vya msingi.
Alisema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha wakulima wanafaidika ipasavyo na mfumo wa stakabadhi ghalani, huku akisisitiza kuwa ushirika umejiandaa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji, uhifadhi, na uuzaji wa mazao hususan ufuta.
Alisema kuwa katika msimu huu, jumla ya maghala 12 yatatumika, ikilinganishwa na maghala tisa yaliyotumika mwaka jana; ikilenga kupunguza changamoto ya mazao kubaki nje wakati wa mnada kutokana na uhaba wa nafasi maghalani.
Alifafanua kuwa wilaya ya Momba itakuwa na maghala matatu wakati eneo la Songwe litakuwa na maghala 10 kwa ajili ya mikusanyiko, akiongeza kuwa matumizi ya mizani ya kidijitali yatatiliwa mkazo ili kuongeza uwazi na ufanisi katika uzani wa mazao.
Mkuu wa wilaya ya Songwe, Fadhiri Nkulu, alisema mkoa una eneo linalofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali la hekta milioni 1.9, ambapo hekta asilimia 85.6 zinafaa kwa kilimo cha zao la ufuta.
Alisema uzalishaji kwa hekta moja unapaswa kutoa tani 1.5, lakini kwa sasa tani 0.5 zinazalishwa, jambo ambalo ni tofauti na malengo ya serikali.
Bw. Nkulu alisisitiza umuhimu wa mfumo wa stakabadhi za maghala katika kuhakikisha wakulima wanapata bei zinazostahili, masoko ya uhakika pamoja na kuongeza thamani ya mazao yao.
Mipango ya baadaye
Akizungumzia mipango ya baadae kuhusu zao hilo, bosi wa COPRA Mlola alisema mamlaka itaongeza uwekezaji katika usambazaji wa mbegu bora na pembejeo, sambamba na kuboresha ufanisi wa huduma za ugani ili kuongeza tija na ubora wa bidhaa zitakazozalishwa.
“Tutaongeza jitihada katika kuimarisha ubora wa ufuta kwa kuwezesha upatikanaji wa mashine za kuchambua, ili bidhaa zinazoingia sokoni zikidhi viwango na madaraja yanayohitajika na wanunuzi wa ndani na kimataifa,” alisema.