KVZ imesema kwa sasa kikosi hicho kipo chini ya Kocha Msaidizi, Ali Khalid Omar’Kisoda’ hadi taarifa nyingine itakapotoka.
Hayo yameelezwa na Ofisa Habari wa KVZ, Abduljalil Mohammed wakati akizungumza na Mwanaspoti ilipotaka kufahamu kikosi hicho kinanolewa na nani baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Malale Hamsini kudai ameachana nao.
Jalil amesema timu hiyo bado haijachana na Malale na kocha huyo yupo nje ya timu kutokana na changamoto za kifamilia zinazomkabili.
“Timu ipo chini ya Kocha Kisoda kwa sasa hadi Malale atakapokuwa sawa na majukumu yote yatakuwa kwake hadi tutakapotoa taarifa,” amesema.
Malale alijiunga na KVZ Desemba 2025 baada ya kuachana na Mbeya City na alianza kuiongoza katika Kombe la Mapinduzi 2026.
Kabla ya KVZ kuchukuliwa na Malale, Kisoda alikuwa akiinoa timu hiyo kwa miaka tisa mfululizo na msimu wa 2024-2025 ilimaliza Ligi Kuu Zanzibar nafasi ya pili ikipigwa bao na Mlandege iliyotwaa ubingwa.
Awali, Malale amesema ameachana na timu hiyo kwa makubaliano maalumu ya kimkataba na uamuzi huo ulikuwa wa manufaa kwa pande zote mbili wala hakuna tatizo kati yao.
Mechi ya mwisho Malale kuiongoza KVZ ilikuwa dhidi ya Azam kwenye Kombe la Muungano na kikosi chake kilipoteza kwa mabao 2-0.