Akizungumza mjini Geneva Uswisi hii leo baada ya kurejea kutoka ziara ya wiki moja nchini Somalia, Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Matthew Hollingworth amesema mamilioni ya Wasomali sasa wanakabiliwa na viwango vya hatari vya njaa baada ya misimu mitatu mfululizo ya mvua kushindwa kunyesha.

“Hii siyo tahadhari ya mbali. Huu ni mgogoro unaoendelea sasa hivi na unazidi kuwa mbaya kwa haraka,” amesema Hollingworth. “Familia nyingi zimeacha kila kitu nyuma ili kwenda kusaka chakula, maji na msaada.”

Mamilioni katika hatari ya njaa kubwa

Kwa mujibu wa WFP, “takribani watu milioni sita nchini Somalia sawa na mtu mmoja kati ya watatu wanakabiliwa na njaa kali, huku watu milioni mbili tayari wakiwa katika kiwango cha dharura, hatua moja kabla ya baa la njaa rasmi kutangazwa.”

Aidha watoto milioni 1.9 wanakadiriwa kuwa na utapiamlo mkali, huku mamia ya maelfu yao wakiwa katika hatari ya aina mbaya zaidi za utapiamlo.

Hollingworth amesema maeneo mengi hasa Puntland yameshuhudia vyanzo vya maji vikikauka kabisa, masoko yakidorora na mifugo pamoja na mazao kuangamia kutokana na ukame wa muda mrefu.

Familia zakimbia makazi yao kutafuta msaada

Katika mji mkuu wa Mogadishu, Hollingworth amesema alikutana na familia moja iliyowasili wiki moja iliyopita kutoka kusini mwa Somalia baada ya kupoteza kila kitu kutokana na njaa na ukosefu wa maji.

“Hata kama mvua zimeanza kunyesha katika baadhi ya maeneo na kuleta matumaini, bado hazijaleta nafuu kwa watu ambao tayari wamepoteza kila kitu,” amesema.

Ameeleza pia kuwa migogoro na ukosefu wa usalama vinaendelea kuzuia upatikanaji wa misaada pamoja na biashara, hali inayozidi kudhoofisha maisha ya watu walio hatarini zaidi.

Uhaba wa fedha wazidisha mateso

WFP imesema ukosefu mkubwa wa fedha umeilazimu kupunguza kwa kiasi kikubwa misaada inayotolewa nchini humo.

“Kwa sasa WFP inawafikia mtu mmoja tu kati ya watu 10 wanaohitaji msaada wa chakula,” amesema Hollingworth.

Akiwa Puntland, amesema alitembelea kituo cha afya ambapo alikutana na akina mama waliotembea mamia ya kilomita kutafuta matibabu kwa watoto wao wenye utapiamlo.

“Mama mmoja aliniambia mtoto wake wa miaka mitatu alikuwa akipata matibabu ya utapiamlo kwa miezi miwili, lakini sasa ameambiwa hakuna msaada mwingine baada ya mwezi huu,” amesema huku akiongeza kuwa “Sasa anajiuliza atawalishaje watoto wake mwezi ujao.”

Kwa mujibu wa Hollingworth, mwaka jana eneo hilo lilikuwa na vituo 12 vya afya vinavyotoa huduma za lishe, lakini sasa ni vituo vitatu pekee vilivyobaki kufanya kazi.

Dunia yaonywa isisubiri janga litokee

Hollingworth amekumbusha kuwa mwaka 2022 Somalia ilikuwa karibu kutumbukia katika baa la njaa kutokana na ukame mkubwa, lakini hatua za haraka zilizochukuliwa na jumuiya ya kimataifa zilisaidia kuzuia maafa hayo.

“Uzoefu wa mwaka 2022 ulithibitisha mambo mawili, kwanza, baa la njaa linaweza kuzuilika; pili, kinga yake ni kuchukua hatua kwa wakati,” amesema.

Amesisitiza kuwa WFP tayari ina mifumo ya kuwafikia watu walio hatarini, ikiwa ni pamoja na watu milioni 1.7 waliosajiliwa kwa mfumo maalum kwa ajili ya kupokea msaada wa fedha taslimu.

Msisubiri hadi iwe janga kubwa

WFP imezitaka serikali na wafadhili kuongeza msaada wa haraka kabla hali haijageuka kuwa janga kubwa zaidi la kibinadamu.

“Ujumbe wetu leo ni rahisi, Tafadhali msisubiri. Chukueni hatua sasa kabla hali hii haijageuka kuwa janga,” amesema Hollingworth. “Dalili zote za hatari nchini Somalia zinaonekana wazi. Njaa inaongezeka, uwezo wa jamii kukabiliana na hali unaanguka, na dirisha la kuzuia janga hili linaendelea kufungwa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *