Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza, Azam FC imepoteza mechi ya Ligi Kuu msimu huu baada ya leo Ijumaa, Mei 8, 2026 kupokea kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa TRA United kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

Waliochangia kuifanya TRA United iharibu rekodi ya Azam FC kutopoteza mechi ya Ligi msimu huu ni Ammy Mapaka ambaye amepachika mabao mawili pamoja na Ally Ng’anzi na Salum Ramadhan ‘Chobwedo’ ambao kila mmoja amefunga bao moja.

Bao la kufutia machozi la Azam FC katika mchezo huo limefungwa na Jephte Kitambala.

Kitambala ndiye aliyeanza kuchokoza mzinga wa nyuki baada ya kufunga bao katika dakika ya sita ya mchezo akimaliza kwa shuti la mguu wa kulia pasi ya kichwa ya Sadio Kanoute.

Bao hilo lilidumu kwa dakika 13 tu kwani Ng’anzi aliisawazishia TRA United katika dakika ya 19 akimaliza mpira uliopigwa kwa kichwa na Ammy Mapaka.

Dakika ya 40, Ammy Mapaka akaifungia TRA United bao la pili akiunganisha kwa kichwa Issack Mtengwa na mshambuliaji huyo akafunga bao la tatu katika dakika ya 43 kwa kichwa tena akimalizia krosi ya Mtengwa tena.

Mabao hayo matatu ya TRA United yalidumu hadi filimbi ya kuashiria muda wa mapumziko ilipopulizwa.

Chobwedo aliihakikishia ushindi TRA United katika dakika ya 62 baada ya kuifungia bao la nne kwa mkwaju wa faulo alioupiga na kisha kuokolewa vibaya na kipa wa Azam FC, Aishi Manula.

Siku mbaya kwa Azam FC katika mchezo huo imejidhihirisha katika dakika ya 69 baada ya kiungo wake Feisal Salum ‘Fei Toto’ kukosa mkwaju wa penalti uliookolewa na kipa Jean Noel wa TRA United.

Matokeo hayo yameifanya Azam FC iendelee kusalia katika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi na point zake 43.

TRA United yenyewe kwa ushindi huo imesogea hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 33.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *