Iringa. Vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na kukosekana kwa maadili kwa baadhi ya watumishi wa umma vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia wananchi kucheleweshewa huduma muhimu na kudhoofisha maendeleo, huku viongozi wa serikali mkoani Iringa wakitakiwa kusimamia uwajibikaji na haki katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza Mei 8, 2026 katika semina ya maadili kwa wakuu wa taasisi na maafisa waandamizi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, RC James amesema rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo na lazima ipingwe kwa nguvu zote.

Semina hiyo iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Iringa pamoja na Sekretarieti ya Maadili ilikuwa na kaulimbiu isemayo “Umuhimu wa kuzingatia maadili katika utumishi wa umma.”

“Rushwa inaweza kumuinua mtu wa hovyo na kumshusha mtu wa chini. Hata serikalini mtu mbabaishaji anaweza kuonekana mzuri huku yule mwema akionekana mbaya kutokana na vitendo vya rushwa,” amesema RC James.

RC James amesema watumishi wa umma wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi wote wanaohitaji huduma serikalini.

Aidha, amewataka wafanyakazi wa mapokezi katika taasisi mbalimbali kuacha tabia ya kuwauliza wananchi maswali mengi yasiyo ya lazima kabla ya kuwafikisha katika ofisi husika kwa huduma.

Wakuu wa Taasisi na maafisa waandamizi kutoka taasisi na Halmashauri mbalimbali mkoani Iringa wakisikiliza semina ya maadili iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa mkoa huo. Picha na Christina Thobias

“Wananchi wanapofika ofisini wanahitaji kuhudumiwa kwa heshima na usawa. Haiwezekani ofisi fulani ikahudumia wananchi wa aina moja tu, hilo halikubaliki,” amesema.

RC James amesema matendo ya watumishi wa umma yanapaswa kuakisi haki, uwajibikaji na uadilifu ili kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao.

Ameeleza kuwa rushwa ina madhara makubwa katika utekelezaji wa mipango ya serikali kwani husababisha kuchelewa kwa huduma za msingi pamoja na kudhoofisha maendeleo ya wananchi.

Kwa mujibu wa RC James, mtu mmoja anayetoa au kupokea rushwa anaweza kuwa chanzo cha kuendelea kwa matatizo makubwa ndani ya taasisi na kuharibu mifumo ya utendaji kazi serikalini.

Amesema serikali inaendelea kutoa elimu ya maadili kwa viongozi na watumishi wa umma ili kuwajengea uwezo wa kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao za kazi.

“Majukumu tunayowapa lazima yaishi kwa kuzingatia utaratibu, sheria na maadili ya utumishi wa umma,” amesisitiza.

RC James pia amegusia aina mbalimbali za maadili ikiwemo maadili ya kitaaluma, kijamii, kisheria pamoja na maadili ya makubaliano ambayo alisema ni muhimu katika kujenga taswira nzuri ya viongozi na taasisi zao.

Amesema maadili ya kijamii hujengwa katika familia, jamii, nyumba za ibada na maeneo mengine ya kijamii, hivyo viongozi wanapaswa kuwa mfano bora kwa wananchi wanaowaongoza.

Katika hatua nyingine, amewakumbusha viongozi wa umma kuwa hakuna anayekatazwa kumiliki mali nyingi, lakini ni muhimu kueleza mali hizo zimepatikanaje kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, amesema semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo viongozi hao ili wawe mabalozi wa maadili na uwajibikaji katika taasisi wanazoziongoza.

Kwa upande wake, Leonard Simba kutoka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma amesema baadhi ya maadili yasiyokubalika katika utumishi wa umma ni pamoja na ulevi wa kupindukia, matumizi mabaya ya madaraka na vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya kazi.

Simba amesema mada kuu ya semina hiyo ilikuwa ni mambo ya msingi katika kanuni za maadili ya utumishi wa umma huku akiwataka viongozi kuwa waadilifu na waaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoani Iringa, Victor Swela akizungumza umuhimu wa semina ya maadili kwa wakuu wa taasisi na maafisa waandamizi mkoani humo. Picha na Christina Thobias

Washiriki wa semina hiyo kutoka taasisi mbalimbali za serikali na halmashauri wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata wakisema itawasaidia kuongeza uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Zainab Mlawa amesema atahakikisha elimu hiyo inawafikia watumishi wote wa manispaa ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, Robert Masunya amesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka kwani yatawasaidia watumishi wa umma kutambua wajibu wao katika kupambana na rushwa na kuimarisha maendeleo ya wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *