Morogoro. Kijana mwenye ulemavu wa mikono anayefanya shughuli zake kwa kutumia miguu, Hamisi Nguku amehitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Kilosa baada ya kumaliza mitihani ya Taifa Mei 8 kwa msaada wa KALAMU Education Foundation (KEF).

Nguku ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Munga, Kata ya Mtimbila wilayani Malinyi, alipata msaada huo baada ya kampuni ya Mwananchi Communications Limited kuchapisha habari kuhusu changamoto za maisha yake na hali yake ya ulemavu.

Changamoto hizo zilimfanya ashindwe kumudu gharama za sare, vifaa vya shule na mahitaji mengine licha ya kufaulu kidato cha nne kwa division two katika mchepuo wa HGK.

Akizungumza baada ya kumaliza mitihani hiyo, Nguku amesema mitihani ilikuwa ya kawaida na ameifanya kwa umakini mkubwa, akiamini kuwa atafaulu vizuri na kupata daraja A litakalomwezesha kuendelea na elimu ya juu.

Mwanafunzi Hamisi Nguku (kushoto) mwenye ulemavu wa mikono, akitumia miguu kuandika baada ya kumaliza Mtihani wa Taifa leo Mei 8, 2026 katika Shule ya Sekondari Kilosa. Pembeni ni mwalimu wake, Mariam Msemakweli, huku akisaidiwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya KALAMU Education Foundation (KEF). Picha na Hamida Shariff.

Aidha, amesema msaada alioupata kupitia KEF umebadilisha maisha yake, akieleza kuwa bila habari yake kuchapishwa na Mwananchi, yeye pamoja na familia yake wasingeweza kumudu gharama za kuendelea na masomo.

“Kwa kweli nilishakata tamaa ya kuendelea na masomo hasa ukizingatia hali duni ya familia ninayotoka. Mama yangu alifariki nikiwa na umri mdogo na baba alikuwa mbali na maisha yangu, hivyo nilikuwa nikilelewa na bibi mzaa mama ambaye ni mzee anayehitaji kusaidiwa,” amesema Nguku.

Ameongeza, “Nashukuru kampuni ya Mwananchi kwa kuchapisha habari zangu ambazo zimeigusa taasisi ya Kalamu Education Foundation (KEF), ambao kwa moyo wao wa imani waliweza kunisaidia kuendelea na masomo yangu ya kidato cha tano na sita. KEF imeweza kunisaidia vitu vingi na naamini wataendelea kunisaidia. Mimi nawahakikishia na kuwaahidi kuwa sitawaangusha kwenye matokeo yangu. Nitafaulu na nitafika chuo kikuu.”

Akieleza hali ya ulemavu wake, Nguku amesema amezaliwa na ulemavu huo ambapo mikono yote miwili imelemaa na haiwezi kufanya kazi wala kushika kitu chochote, hivyo amekuwa akitumia miguu kwa kuandika, kula, kufua na kufanya kazi nyingi, japokuwa zipo kazi ambazo hawezi kufanya kwa kutumia miguu. Hivyo, amekuwa akipata msaada kutoka kwa wanafunzi wenzake, walimu na jamii inayomzunguka.

“Mfano kubeba ndoo ya maji, kuoga, kutandika kitanda ama kunyanyua vitu vizito siwezi. Wakati nakua, nilipofikia umri wa kujitambua na kujikuta ni mlemavu, kiukweli nilijiona mnyonge na sifai kwenye jamii. Lakini baada ya kupelekwa shule na kuona nafanya vizuri darasani, nilijiona mimi ni binadamu kama wengine na naweza kusoma na kufanya vitu kulingana na ulemavu wangu.”

Ameongeza, “Baada ya kutembea kwenye maeneo mbalimbali zikiwemo ofisi za umma na binafsi na kukuta watu wenye ulemavu wakifanya kazi na kuaminiwa, imenipa moyo na nguvu ya kusoma huku nikiamini ipo siku na mimi naweza kuajiriwa ama kujiajiri kupitia taaluma yangu.”

Kijana Hamisi Nguku akila chakula kwa kwa kutumia mguu wakati Mwananchi ilipomtembelea nyumbani kwao Morogoro. Picha na Maktaba

Ameeleza ndoto zake ni kusoma hadi kufikia ngazi ya PhD na kuwa mtangazaji mahiri kwenye vituo vikubwa vya redio ama televisheni hapa nchini ama nje ya nchi, hasa kwenye vipindi vya kijamii vinavyogusa maisha ya watu hususan wenye uhitaji.

“Naipenda sana kazi ya uandishi wa habari hususan eneo la utangazaji kwa sababu mimi ulemavu wangu ni wa mikono, hivyo kazi hii ya utangazaji itanifaa kwa vile nitakuwa natumia mdomo kuzungumza,” amesema Nguku.

Akieleza maisha ya Nguku nje ya masomo, mwalimu wa Shule ya Sekondari Kilosa, Mariam Msemakweli amesema mwanafunzi huyo pia ana kipaji cha kuchora na hushiriki michezo, burudani pamoja na shughuli nyingine kulingana na uwezo wake, huku akiwa mwenye furaha muda wote.

Msemakweli amesema Nguku alijiunga na shule hiyo mwaka 2024 akiwa kidato cha tano na aliweza kuzoea mazingira pamoja na wanafunzi wenzake kwa haraka. Katika kipindi chote cha miaka miwili, amekuwa mwanafunzi mnyenyekevu, anayejitambua na mwenye kufanya vizuri katika masomo yake.

Amesema ana imani kuwa atafanya vizuri katika mitihani ya Taifa iliyoanza Mei 5.

Aidha, ameiomba KEF kuendelea kumsaidia mwanafunzi huyo hadi atakapopata nafasi ya kujiunga na elimu ya juu ili aweze kutimiza ndoto zake na kusaidia familia yake pamoja na bibi yake.

Kwa upande wake, mwakilishi wa KEF, Mohamed Kamilagwa ameipongeza Mwananchi Communications Limited kwa kuchapisha habari ya Hamisi Nguku, jambo lililoigusa taasisi hiyo na kuamua kutoa msaada. Pia ameushukuru uongozi wa shule hiyo kwa kuwathamini wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

“Mbali na kumsaidia kuanzia kidato cha tano hadi sita, tutaendelea kumsaidia katika elimu ya juu.

“Ulemavu si lazima mtu azaliwe nao, unaweza kumpata mtu wakati wowote. Tunamthamini kijana huyu na tunaamini changamoto zake za kimaumbile hazitazuia kutimiza ndoto zake,” amesema Kamilagwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *