Mbeya. Kutokana na kuporomoka uzalishaji wa zao la pareto, Serikali mkoani Mbeya imekuja na mikakati ya kufanya msako wa kudhibiti mianya ya utoroshwaji unaofanywa na baadhi ya wanunuzi wa makampuni kwa kutumia usafirishaji wa bodaboda.

Imeelezwa hali hiyo imesababisha kupungua kwa ubora kutoka wastani wa asilimia 2.3 hadi moja, licha ya mikakati ya wadau na Serikali kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa ubora.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbeya, Cuthbert Mwinuka, leo Jumamosi Mei 9, 2026, kwenye mkutano uliohusisha mawakala wa Kampuni ya Pareto PCT wenye lengo la kufanya tathmini ya uzalishaji kwa mwaka 2025 na mikakati kwa mwaka 2026.

“Tumebaini kuwepo kwa baadhi ya makampuni ambayo hayajajidhatiti kuwekeza kwa wakulima na badala yake kuingia mashambani kuwarubuni wakulima kwa kununua pareto kavu na mbichi, ikiwa ni pamoja na kutorosha kwa kutumia usafiri wa bodaboda, jambo ambalo ni kosa kisheria,” amesema.

Amesema wamejipanga kufanya msako katika maeneo mbalimbali yanayotajwa kutumika kutorosha pareto kwa kuwakamata watakaobainika na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Amesema ni jambo la kushangaza kwamba katika halmashauri hiyo kuna makampuni 10 yanayonunua pareto, lakini kati ya hayo, matatu pekee yana mchango mkubwa wa kuwekeza kwa wakulima.

“Serikali haitaweza kuvumilia tabia ya utoroshwaji wa zao hilo kuendelea wakati ikiweka mikakati mbalimbali ya kuhamasisha wakulima kutumia mbinu bora za uzalishaji ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.”

Amesema ili kuongeza tija ya uzalishaji, Kampuni ya PCT kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI-Uyole), imetoa mbegu bora za pareto kilo milioni 5.7 kwa lengo la kuwezesha kufikia malengo ya kukusanya kilo milioni sita kwa msimu wa mwaka 2026, huku PCT wakilenga kilo milioni 2.5.

Mikakati ya kunusuru zao hilo

Ametaja miongoni mwa mikakati ni kuelekeza makampuni yatakayojidhatiti kwenye ununuzi wa zao hilo kuwekeza nguvu kwa wakulima ili kuongeza tija kubwa ya uzalishaji badala ya kutegemea migongo ya wengine.

Mikakati mingine ni kutoa elimu kwa wakulima kutumia maelekezo ya wataalamu wa kilimo kwa kupanda miche kwa wakati ili msimu ujao kuzalisha maua yenye sumu yenye ubora sokoni.

Katika hatua nyingine, Mwinuka amesema wastani wa uzalishaji kwa mwaka unapaswa kuwa kilo milioni 13 ambazo zitakidhi mahitaji ya viwanda vitatu, huku kampuni ya PCT pekee ikihitaji kilo milioni sita.

“Tulifanya kikao cha wadau kujadili mikakati ya kuhakikisha ndani ya miaka mitatu tunafikisha kilo milioni 13, sambamba na kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vikaushio 40,” amesema.

Kauli ya kampuni ya ununuzi

Akizungumzia athari ya kushuka kwa uzalishaji, Mhasibu Mkuu wa Kampuni ya Pareto PCT, Edesius Mbegu amesema kwa msimu wa mwaka jana wamepata hasara ya Sh milioni 500 kutokana na sababu mbalimbali.

Amesema waliweka malengo ya kununua pareto kilo milioni 1.7, lakini wamepata kilo milioni 1.442 sawa na asilimia 70, jambo ambalo limewapa hasara kwa msimu wa mwaka 2025.

Amesema kwa msimu wa 2026 wanatarajia kununua kilo milioni 2.5 ili kukidhi mahitaji ya kiwanda sambamba na kuwataka wakulima kuhakikisha pareto inakuwa na sumu ya kiwango cha asilimia 1.4 huku unyevu usizidi asilimia 15.

Kwa upande wake, Ofisa Pareto wa Mikoa ya Mbeya na Songwe, Musa Malubalo amesema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya uzalishaji kwa mwaka 2025 na mikakati ya mwaka 2026.

Amesema kwa msimu uliopita walikumbana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa mwanzoni mwa msimu kuanzia Novemba mwaka jana kutokana na kutokuwepo kwa mvua za kutosha.

“Lakini kuelekea mwishoni mwa msimu tulipata mvua nyingi ambazo ziliathiri mashamba. Kwa msimu wa 2026 tumekuja na mikakati ya kuboresha vikaushio vya pipa 386 na vingine vitatu vya kisasa vyenye uwezo wa kukausha kilo 10 za pareto kwa wakati mmoja.”

Amesema kupitia mikakati hiyo itasaidia wakulima kuzalisha kwa ubora, hususan kukausha kwa muda mfupi, sambamba na kushirikiana na Kituo cha TARI-Uyole kuandaa mbegu bora kilo 5,788 za zao la pareto.

Malubalo amesema matarajio kwa msimu ujao ni wakulima wa mikoa ya Mbeya na Songwe kuzalisha kilo milioni 2.5.

Naye Mtafiti wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI-Uyole), Rachel Ndala amesema tayari wamezalisha mbegu za aina nne za zao la pareto ambazo zitakuwa na tija na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Tunashauri wakulima kuzingatia tija kubwa na ubora katika uzalishaji ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema.

Naye Edwin Andrew, Ofisa Kilimo wa Copra, amewataka mawakala kuzingatia maelekezo hususan matumizi ya mizani ya kielektroniki na kuwepo kwa bei elekezi ya zao hilo huku akiahidi kufanya ukaguzi.

Kwa upande wa mawakala walioshiriki kikao hicho, wameomba Serikali kuingilia kati kudhibiti wanunuzi holela ambao wamekuwa kikwazo na kushusha uzalishaji wa zao hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *