Katika ujumbe wake wa moja kwa moja kwa wakazi wa Tenerife ulioutoa hii leo akiwa Madrid, Hispania Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema anaelewa hofu ya wananchi hao kutokana na kumbukumbu za mlipuko wa coronavirus“>COVID-19, lakini akasisitiza kuwa hali ya sasa ni tofauti.

“Hii si COVID nyingine. Hatari ya sasa ya kiafya kutokana na hantavirus bado iko chini,” amesema Tedros.

Kwa mujibu wa WHO, virusi vilivyopo kwenye meli hiyo ni aina ya Andes hantavirus na kwamba kwa sasa hakuna abiria wenye dalili za ugonjwa huo ndani ya meli hiyo. 

Tayari mtaalamu wa WHO yupo ndani ya meli hiyo kufuatilia hali hiyo.

Tedros kwenda Tenerife

Mkuu huyo wa WHO amesema anatarajia kwenda Tenerife mwenyewe kushuhudia operesheni hiyo na kutoa shukrani kwa wananchi wa kisiwa hicho kwa mshikamano na huruma waliyoonesha.

Ameeleza kuwa mamlaka za Hispania zimeandaa mpango maalum wa kuwashusha abiria kupitia bandari ya viwanda ya Granadilla, mbali na maeneo ya makazi ya watu, kabla ya kuwarejesha moja kwa moja katika nchi zao.

“Tenerife imechaguliwa kwa sababu ina uwezo wa kitabibu, miundombinu na ubinadamu wa kusaidia watu hao kufika salama,” amesema Tedros.

Shirika hilo limesema watu watatu wamefariki dunia kutokana na maambukizi hayo, huku likitoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *