
Kufuatia kupunguzwa kwa vikwazo vilivyokuwa vinaikabili sekta ya mafuta, Iran imesafirisha takriban mapipa milioni 50 ya mafuta katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, na inakadiriwa kuwa imepata mapato yanayozidi dola bilioni 3.5 za Kimarekani.
Kwa mujibu wa ripoti ya TankerTrackers, Iran imeongeza mauzo yake ya mafuta tangu takribani wiki mbili zilizopita, baada ya kuondolewa mzingiro uliowekwa na Marekani. Katika kipindi hicho, imeuza takribani mapipa milioni 50 ya mafuta ghafi katika masoko ya kimataifa.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, wastani wa mauzo ya mafuta ya Iran katika mwezi Juni 2026 ulifikia takribani mapipa milioni 1.66 kwa siku. Hali hii inakuja wakati ambapo mauzo ya mafuta ya nchi nyingi za eneo hilo bado hayajarejea katika kiwango kilichokuwapo kabla ya mivutano ya hivi karibuni kati ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.
Wataalamu wa soko la nishati wanakadiria kuwa, mauzo ya mapipa milioni 50 ya mafuta katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, kwa kuzingatia bei za hivi karibuni za mafuta katika soko la kimataifa, yameiingizia Iran mapato ya takribani dola bilioni 3.5 za Marekani. Hivyo, wastani wa mapato ya kila siku ya Iran kutokana na mauzo ya mafuta katika kipindi hicho unakadiriwa kuzidi dola milioni 233.
Katika muktadha huo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mkuu wa timu ya mazungumzo ya Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, alisema katika mahojiano ya televisheni yaliyofanyika jana usiku kuwa, vikwazo vya mafuta vimeondolewa, na kwamba kwa sasa Iran inauza mafuta yake kwa bei iliyo juu kwa takribani asilimia 20 ikilinganishwa na hapo awali.