
Mkuu wa timu ya Iran ya mazungumzo na Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaingia katika mazungumzo yoyote mapya na Marekani mpaka masharti yote yaliyomo katika hati ya makubaliano ya maelewano iliyopo yatakapotekelezwa kikamilifu.
Qalibaf amesisitiza katika mahojiano na televisheni ya taifa ya Iran kwamba, Tehran inashikilia kwa dhati mamlaka yake ya kitaifa na haki zake katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, akibainisha kuwa kipindi cha kupita bila malipo ni siku sitini pekee.
Ameeleza kuwa mikutano inayoendelea hivi sasa inalenga kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizomo katika hati ya makubaliano ya maelewano iliyosainiwa kati ya Iran na Marekani.
Spika wa Bunge la Jamhuuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza pia kwamba, mazungumzo yoyote mapya hayawezi kuanza kabla ya utekelezaji kamili wa makubaliano yaliyokwisha kufikiwa, akifafanua kuwa mikutano ya sasa haimaanishi kufunguliwa kwa duru mpya ya mazungumzo.
Kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz, Qalibaf amesema kuwa Iran ina mamlaka ya pamoja juu ya mlango huo sambamba na Oman, akisisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitawahi kuachia haki zake katika eneo hilo.
Aidha, aliongeza kuwa ruhusa ya kupita bila malipo katika Mlango wa Bahari wa Hormuz imewekewa ukomo wa siku 60 pekee, akieleza kuwa kipengele hicho kinahusiana na muda uliobainishwa katika hati ya makubaliano ya maelewano.