
Dar es Salaam. Coop Bank imezindua tawi jipya mjini Mtwara ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kupanua huduma za kifedha nchini na kuimarisha uchumi jumuishi.
Uzinduzi huo uliofanyika mwishoni mwas wiki umeifanya benki hiyo, ambayo imekaa sokoni kwa mwaka mmoja pekee, kufikisha matawi matano yaliyopo Dodoma, Moshi, Tabora, Tandahimba na Mtwara. Aidha, benki hiyo imetangaza kuwa hivi karibuni itafungua tawi jingine jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Donald Msengi, aliipongeza benki hiyo kwa kuendelea kuwekeza katika mkoa huo na kusema hatua hiyo inaonesha imani kubwa waliyonayo kwa wananchi wa Mtwara.
Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan wa maeneo ya vijijini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Joseph Witts, alisema ufunguzi wa tawi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kusogeza huduma karibu na wananchi kwa lengo la kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na ustawi wa jamii.
Alibainisha kuwa Mkoa wa Mtwara una mchango mkubwa katika uchumi wa taifa kupitia zao la korosho, jambo lililoifanya benki kuona umuhimu wa kuwekeza katika eneo hilo kutokana na fursa zilizopo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ngu’urah, alisema benki imejipanga kufungua matawi mengine matatu katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera na Mwanza kabla ya mwisho wa robo ya tatu ya mwaka huu.
Alisema ndani ya mwaka mmoja benki hiyo imepata mafanikio makubwa na kuongeza idadi ya wateja kutoka 5,000 hadi zaidi ya 37,000, hatua inayoonesha kuongezeka kwa imani ya wananchi na kupanuka kwa huduma zake.