Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Mama Duniani, macho na mioyo hugeukia wanawake wanaobeba uhai, kuuvumilia uchungu wa uzazi na hatimaye kuleta maisha mapya duniani.
Ni siku ya kutafakari ujasiri wa mama, lakini pia ni siku ya kuangalia jinsi sayansi ya tiba inavyoboresha uzoefu wa uzazi ikiwamo matumizi ya sindano ya ganzi ya uti wa mgongo ‘epidural’ kwa mama wanaojifungua kwa upasuaji.
Epidural ni aina ya ganzi ya sehemu ya mwili inayotolewa kwa kutumia sindano maalumu iitwayo ‘epidural needle’. Sindano hii huingizwa kwa uangalifu katika eneo la mgongo wa chini, kwenye nafasi inayoitwa epidural space.
Baada ya hapo, bomba jembamba huachwa mahali hapo ili dawa ya ganzi iendelee kutolewa taratibu. Dawa hii huzuia maumivu kutoka sehemu ya kiunoni kwenda chini bila kumlaza mama usingizi mzito, hivyo kumruhusu kubaki macho na kushiriki katika tukio la kuzaliwa kwa mtoto wake.
Kwa mama wanaojifungua kwa upasuaji, sindano hiyo hutumika kama njia mbadala salama ya ganzi, ikilinganishwa na ganzi ya kulala kabisa.
Faida yake kubwa ni kwamba mama hubaki na ufahamu kamili wa kinachoendelea, lakini bila kuhisi maumivu ya upasuaji.
Mwonekano wa sindano ya ganzi ya uti wa mgongo ‘epidural’ yenye urefu wa takribani sentimita 8 hadi 10 ikilinganishwa na sindano ya kawaida yenye sentimita 1.5 hadi 4
“Nilisikia mtoto wangu akitoka bila maumivu,” amesema Rehema Kundi (30), mkazi wa Kinondoni, aliyejifungua kwa upasuaji baada ya kugundulika mtoto wake alikuwa katika mkao usio sahihi tumboni.
“Nilikuwa na hofu sana nilipoambiwa nitafanyiwa upasuaji. Lakini daktari aliniambia nitapewa epidural, sitasikia maumivu lakini nitabaki macho,” amesema.
Rehema anasema aliwahi kusikia kuhusu sindano hiyo, hivyo alipotakiwa kuchomwa alikuwa na wasiwasi kuhusu mgongo wake.
Hata hivyo, baada ya epidural kuanza kufanya kazi, alihisi ganzi ikienea polepole sehemu ya chini ya mwili wake.
“Nilihisi kama miguu yangu imekuwa mizito na haisikii kitu. Lakini sikuwa na maumivu kabisa. Nilikuwa natulia tu na kusubiri,” amesema.
Dakika chache baadaye, upasuaji ulianza. Rehema anasema alisikia mazungumzo ya madaktari, lakini hakuhisi maumivu yoyote.
“Kilichonigusa zaidi ni niliposikia mtoto wangu akilia. Nilijua amezaliwa salama. Nililia kwa furaha,” ameongeza.
Fatma Ally (27), mama wa pacha, naye alijifungua kwa upasuaji wa dharura baada ya matatizo ya uzazi kuonekana wakati wa uchungu.
“Nilikuwa na hofu kubwa sana. Nilidhani nitalala kabisa na sitajua kinachoendelea,” amesema.
Lakini, madaktari walimweleza kuhusu sindano hiyo na jinsi inavyofanya kazi. Baada ya ridhaa yake, sindano iliwekwa mgongoni na dawa ikaanza kufanya kazi.
“Nilihisi ganzi kuanzia kiunoni kwenda chini, lakini nilikuwa macho kabisa. Nilikuwa nasikia kila kitu kinachoendelea,” amesema.
Anakumbuka wazi jinsi alivyoshuhudia watoto wake wakitolewa mmoja baada ya mwingine.
Mwonekano wa sindano ya ganzi ya uti wa mgongo ‘epidural’ yenye urefu wa takribani sentimita 8 hadi 10 ikilinganishwa na sindano ya kawaida yenye sentimita 1.5 hadi 4
“Ilikuwa hisia ya kipekee. Sikuona maumivu, lakini nilihisi kila dakika ya kuwa mama wa pacha. Ilikuwa kama zawadi mbili kubwa maishani mwangu,” amesema.
Daktari bingwa wa usingizi, Dk Yunus Msuya, ameeleza kuwa epidural ni mojawapo ya mbinu muhimu zaidi katika huduma za kisasa za uzazi, hasa kwa upasuaji.
“Sindano hii hutumika kuweka dawa ya ganzi kwenye nafasi ya epidural kwenye mgongo. Dawa hii huzuia hisia za maumivu kutoka sehemu ya chini ya mwili wakati wa upasuaji,” amesema.
Amefafanua tofauti na ganzi ya kulaza kabisa, epidural humruhusu mama kubaki macho na kushiriki katika mchakato wa kuzaliwa kwa mtoto wake.
“Hii ni muhimu sana kisaikolojia. Mama anabaki na kumbukumbu ya moja kwa moja ya kuzaliwa kwa mtoto wake, bila maumivu ya upasuaji,” ameeleza.
Dk Msuya amesisitiza kuwa utaratibu huo hufanywa na wataalamu waliobobea na unahitaji ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.
“Kama ilivyo kwa kila huduma ya kitabibu, kuna tahadhari. Si kila mama anafaa kupatiwa epidural, hivyo tathmini ya kitabibu ni muhimu kabla ya kuitumia,” ameongeza.
Ingawa epidural ni teknolojia ya kitabibu, athari yake kubwa zaidi huonekana katika hisia za mama. Kwa baadhi, huondoa hofu ya upasuaji na kuwapa utulivu, huku wengine huwapa nafasi ya kuwa mashahidi wa moja kwa moja wa kuzaliwa kwa watoto wao