Manchester, England. Kipa wa Manchester United, Senne Lammens ameitaka klabu hiyo kuwekeza vya kutosha katika usajili wake ujao ili iweze kupambana na ratiba ngumu msimu ujao.

Lammmens mwenye umri wa miaka 23 ametoa ushauri huo muda mfupi baada ya timu yake kulazimishwa sare tasa ugenini dhidi ya Sunderland juzi Jumamosi.

Man United tayari imeshajihakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao lakini ilionekana kuzidiwa vilivyo na Sunderland katika mechi hiyo ambayo ilipiga shuti moja tu lililolenga lango.

Na shuti hilo lenyewe lilipatikana katika dakika ya 93 ya mchezo likipigwa na Matheus Cunha.

Kiwango hicho kisicho cha kuvutia na idadi kubwa ya michezo ambayo Man United itakuwa nayo msimu ujao, ni mambo mawili yanayomfanya Lammens raia wa Ubelgiji aitake timu yake kufanya usajili mkubwa ili iweze kushindana msimu ujao.

“Ni ligi ngumu. Mwaka unaofuata utakuwa ni program ngumu. Hivyo unatakiwa kupata watu wengi ndani ambao wataingia pale watakapohitajika.

Hata hivyo Lammens hajasita kupongeza kikosi cha sasa kwa namna ambavyo kimeweza kupambana na kuwepo katika nafasi tatu za juu licha ya changamoto ya majeraha.

Lammens amesema kuwa sio kazi rahisi kufanya vizuri huku ukiwa na wachezaji majeruhi mara kwa mara hivyo timu yake inastahili pongezi.

“Tayari tuna wachezaji wengi wenye ubora kwenye kikosi mwaka huu. Lakini kwa msimu ujao kutakuwa na mambo mengi. Na unatakiwa ujumuishe majeraha na mambo mengine yanayoweza kutokea.

“Tunatakiwa kuwa na kikosi kizuri na imara katika msimu ujao. Tumekuwa tukikua na sasa ni hatua nyingine. Msimu ujao unapaswa kuwa wenye jambo kubwa. Hivyo kila mmoja atapiga hatua.

Kipa huyo amesema kuwa walichokipata msimu huu sio lengo lao kuu hivyo msimu ujao wanatakiwa kufanya vizuri zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *