
China imepinga vikali vikwazo vipya vilivyowekwa na Marekani dhidi ya kampuni zake tatu kwa madai ya kusaidia shughuli za kijeshi za Iran, na imeahidi kulinda biashara zake dhidi ya hatua hizo ambazo imezitaja kuwa za upande mmoja na zisizo halali.
Akizungumza katika mkutano wa kawaida na wanahabari Jumatatu, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Guo Jiakun, alisema Beijing daima imezitaka kampuni zake kufanya biashara kwa kuzingatia “sheria na kanuni.”
Ameongeza kuwa: “Tutasimamia imara kutetea haki halali na masilahi ya makampuni ya China.”
Guo amesisitiza umuhimu wa kutumia kila jitihada kuzuia kurejea kwa vita katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati), akisema hilo ndilo jukumu la dharura zaidi duniani kwa sasa.
Kauli hizi zinakuja kama karipio jipya la Beijing dhidi ya kampeni ya Washington ya kile inachokiita shinikizo la juu dhidi ya Tehran, siku chache tu kabla ya ziara inayotarajiwa ya Rais wa Marekani Donald Trump nchini China.
Wizara ya Fedha ya Marekani imeweka vikwazo dhidi ya watu na kampuni kumi, zikiwemo kampuni kadhaa za China na Hong Kong, kwa madai ya kusaidia Iran kupata silaha na malighafi zinazohitajika kwa ndege zake zisizo na rubani za Shahed pamoja na makombora ya masafa marefu.
Katika hatua isiyo ya kawaida na yenye upinzani wa wazi, China imekabiliana na vikwazo vya Washington dhidi ya viwanda vyake vya kusafisha mafuta ya Iran kwa kutumia “kanuni ya kuzuia” kwa mara ya kwanza, ikiwaamuru wafanyabiashara wake kutotekeleza vikwazo vya Marekani.