Aprili Mosi 2026, shirika la Shirika la Anga na Uchunguzi wa Anga za Juu la Marekani (NASA), lilituma chombo angani kuelekea mwezini.

Kwa muda wa siku kumi, chombo hicho kilichopewa jina Orion, kimekuwa na jukumu la kukusanya habari kuhusu mwezi na anga.

Wanaanga wenye jukumu hilo katika mradi huo uitwao Artemis II, ni Reid Wiseman, Victor Glover, Christina Koch na Jeremy Hansen. Safari hii inafikia umbali ambao haujawahi kufikiwa na binadamu.

Pili, wanaanga hawa wamefanikiwa kuona upande wa mwezi ambao haujawahi kuonekana na binadamu. Upande huo una milima ya miamba na mabonde makubwa.

Inakisiwa kwamba mradi huu utasaidia katika kumwezesha binadamu kufikia sayari ya Mirihi (Mars) inayodhaniwa kuwa na madini mengi.

Hatua hizi muhimu katika ugunduzi zimefikiwa kutokana na mashindano baina ya mataifa mbalimbali.

Kwa mfano, mwaka 1959 katika mradi ulioitwa Luna 2, Muungano wa Sovieti ulituma chombo mwezini. Mwaka 1966, chombo kilichoitwa Luna 9 kilitua mwezini. Hali hii iliwapa washindani wa Sovieti, yaani Marekani, kiwewe.

Kufikia mwisho wa miaka ya 1960 yaani  mwaka 1969 katika mradi ulioitwa Apollo 11, Marekani ilifaulu kuwatuma wanaanga watatu mwezini ambapo Neil Armstrong na Buzz Aldrin waliandika historia kama binadamu wa kwanza kukanyaga na kutembea mwezini.

Mwenzao Michael Collins alisalia chomboni kwa kuwa ndiye aliyekuwa rubani.

Wanaanga wa Apollo 17 ya Marekani walitua mwezini mwaka 1972 na Wasovieti katika Luna 24 wakawa wa mwisho kufika mwezini mwaka1976.

Muungano wa Sovieti ulisambaratika  mwaka 1991. Kwa kukosa ushindani, safari za kuenda mwezini zilikoma. Ndio sababu imekuwa miaka 54 tangu Wamerekani walipofika mwezini mara ya mwisho.

Lakini sasa mambo yamebadilika. Kuna ushindani mpya. China ina mradi unaoitwa Chang’e na ina lengo la kupeleka wanaanga mwezini kufikia 2030.

Mwaka 2019, kwa kutumia roboti kwenye Chang’e 4, China lilikuwa taifa la kwanza kufika eneo la mbali kabisa la mwezi. Baada ya hapo, roboti za Wachina zilifanya ziara miaka ya 2020 na 2024.

Ni maoni yangu kwamba ziara hizi za Wachina ndizo zilizoigutua Marekani na kwa sasa ni wazi kwamba ushindani umeanza rasmi!

Nimeandika haya kudhihirisha kwamba ushindani baina ya mataifa aghalabu huzaa matunda mema.

Ni kwa mintarafu hii ndipo ninapendekeza kwamba kuwe na ushindani wa kina baina ya Kenya na Tanzania katika kukuza na kukisambaza Kiswahili.

Ushindani huu utakuwa baraka kuu kwa lugha yenyewe.

Tanzania imefanya mengi katika kukuza Kiswahili nyumbani na kimataifa. Ni maoni yangu kwamba iwapo kungekuwa na ushindani katika hili, basi kazi ya kukikuza na kukisambaza ingeongezeka.

Kuhusu Kiswahili, mshindani wa pekee wa Tanzania ninayemuona ni Kenya.

Kenya inafaa itie nia na ionyeshe ari kushindana na Tanzania katika kuasisi vituo vya kufundisha Kiswahili katika balozi zake.

Vilevile, Kenya inafaa kushindana na Tanzania katika shughuli za kibalozi za utambuzi wa Kiswahili.

IkiwaTanzania ilishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kuamua kuwe na Siku ya Kiswahili Duniani, Kenya inaweza kufanya nini?

Vilevile, Kenya inafaa kushindana na Tanzania katika kutuma walimu wa Kiswahili katika mataifa mbalimbali ya Afrika na nje ya bara hili.

Zaidi ya yote, Kenya inafaa kushindana na Tanzania katika kuzindua taasisi na asasi tofauti tofauti zitakazokuza Kiswahili.

Nchini Tanzania kuna mabaraza mawili ya Kiswahili (Bakita na Bakiza) ilhali Kenya hakuna hata moja.

Tanzania kuna taasisi ya masomo ya Kiswahili (Tataki) ilhali Kenya hatuna taasisi kama hiyo.

Kwa hakika, nimeelezwa kwamba serikali ya Tanzania imetoa ardhi ya kujenga chuo kikuu kitakachotambulika na kuimarika katika ufunzaji wa Kiswahili, Kenya je?

Naomba nchi yetu ishindane na jirani wetu kwa hili. Huu utakuwa ushindani chanya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *