Beki wa Simba SC, Rushine De Reuck, amefunguka kuhusu kipindi kigumu alichopitia mwishoni mwa maisha yake ya soka akiwa Mamelodi Sundowns, akisema alikuwa hajui mustakabali wake ulikuwa wapi.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 30 amesema majeraha na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara vilimfanya ashuke kwenye mpangilio wa kikosi cha Sundowns, hali iliyozua mazungumzo magumu kuhusu hatima yake.

Akizungumza Shika la Habari Afrika Kusini (SABC) De Reuck amesema:

“Mwanzoni mwa msimu nilikuwa kwenye mazungumzo na Sundowns kuhusu uwezekano wa kuondoka kwenye timu. Kulikuwa na chaguo mbalimbali ndani ya Afrika Kusini, lakini kipindi hicho kilikuwa kigumu kwangu kwa sababu sikujua nataka kuwa wapi.”

Ingawa Sundowns walikuwa tayari kumbakiza kama mchezaji wa kikosi hicho, De Reuck alihisi bado alikuwa anahitaji nafasi kubwa zaidi ya kucheza kuliko aliyopewa.

Ushawishi wa Fadlu Davids

Mabadiliko makubwa yalikuja baada ya Fadlu Davids kuonyesha nia ya kumtaka Simba.

Kocha huyo wa zamani wa Maritzburg United, ambaye aliwahi kufanya kazi vizuri na De Reuck, ndiye aliyekuwa sababu kuu ya beki huyo kuamua kujiunga na Simba badala ya kubaki Afrika Kusini.

“Kocha Fadlu alipoongea namimi nilijua hii itakuwa nafasi nzuri ya kucheza tena na kurejesha kujiamini kwangu, na pengine kurudi kwenye timu ya taifa,” alisema De Reuck.

“Bado nilitaka kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba walinipa nafasi hiyo, aliongeza

“Fadlu ndiye aliyenipa mkataba wangu wa kwanza wa kitaalamu Maritzburg United, hivyo tuna uhusiano mzuri na nilijua angeweza kunifanya nirudi kwenye ubora wangu wa juu nikifanya kazi chini yake. Sikutaka kuikosa nafasi hiyo.”

Asema huu ni msimu wake bora:

Tangu ajiunge na Simba, De Reuck amesema amerejea kwenye kiwango chake bora na anaamini huu ni mmoja wa misimu yake bora zaidi kisoka.

Amesema kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye klabu ya Simba, kumemsaidia kufufua upya kiwango chake.

“Nafikiri huu ni mmoja wa misimu yangu bora kwa takwimu. Nimeanza michezo 35 katika mashindano yote, nimefunga mabao matatu, nimepata tuzo za mchezaji bora wa mechi na tumeshinda taji,” alisema De Reuck.

Simba kwa sasa ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikivuna pointi 49 ikicheza mechi 22 tofauti ya pointi tano na Yanga inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 54 katika mechi 22.

Katika msimu huu wa 2025/26 Simba imetwaa ubingwa wa Muungano Cup baada ya kuitandika Yanga kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye uwanja wa New Amaan Complex.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *