Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Kassimu Mganga amezungumzia wazi hisia zake kuhusu uhusiano wa mastaa wa Bongo, akisema kuwa kwake Diamond Platnumz na Zuchu ni miongoni mwa kapo zinazovutia zaidi kutokana na namna wanavyoendana kimapenzi na kisanaa.

Akizungumza na Mwananchi, Kassimu amesema alianza kuwa na mtazamo chanya kuhusu wawili hao hata kabla ya uhusiano wao kuwa wazi kwa mashabiki, akihisi kuna kitu cha tofauti kinachowaunganisha.

“Nilikuwa naona kabisa Diamond na Zuchu wanaendana sana. Hata kabla hawajatangaza wazi, nilikuwa tayari naona hawa watu watakuwa kitu kimoja kizuri,” amesema Kassimu.

Msanii huyo amesema moja ya mambo yanayomvutia ni jinsi wawili hao wanavyolingana licha ya tofauti ndogo za umri, akisema hilo linawasaidia kuelewana na kufanya uhusiano wao uwe na mvuto zaidi.
 

“Wanaendana sana kimapenzi na kisanaa na bado ni vijana. Hii inawasaidia sana kuelewana,” aliongeza.

Kassimu pia alimpongeza Diamond Platnumz kwa bidii yake ya kazi, akisema msanii huyo amekuwa mfano wa kujituma na kupambana hadi kufikia mafanikio makubwa katika muziki na biashara.

“Diamond anajua kupambana sana na kutafuta pesa. Hiyo inamfanya awe tofauti na wengi,” amesema.

Amesema uhusiano wa wawili hao umekuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa muziki Tanzania, huku watu wengi wakifuatilia kila hatua yao kwa karibu kutokana na namna wanavyoonekana kuendana.

“Hii couple si ya kawaida, watu wengi sana Tanzania wanaifuatilia na kuipenda,” amesema Kassimu.

Msanii huyo alitania kwa kusema kama kungekuwa na uwezo, angependa hata kuona historia ya mapenzi yao ikihifadhiwa kwa namna ya kipekee kutokana na ukubwa wa ushawishi wao kwa jamii.

“Kama ingewezekana, hata picha ya ndoa yao ingejengewa sanamu kwa sababu ya jinsi watu wanavyowapenda,” amesema.

Aidha, Kassimu ametaja pia wimbo wake wa Awe Nae kuwa miongoni mwa kazi anazozipenda zaidi, akisema humpa furaha kubwa anapouimba jukwaani kutokana na mapokezi mazuri ya mashabiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *