Mbeya. Barabara katika mitaa 181 ndani ya kata 36 za Halmashauri ya Jiji la Mbeya, zinatarajiwa kuboreshwa, baada ya halmashauri hiyo kutumia Sh500 milioni kununua mtambo wa kisasa wa kuchonga miundombinu hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa leo Jumanne Mei 12, 2026, wakati akizungumza na Mwananchi ofisini kwake.
Amesema mpango huo ulianza na majadiliano katika kikao cha baraza la madiwani na baadaye wakakubaliana kununua mtambo huo.
“Tumenunua mtambo wa kisasa wa kuchonga barabara na tayari kazi imeanza katika baadhi ya kata, lengo ni kufikia kata zote 36 na mitaa yote yenye changamoto,” amesema.
Amesema lengo ni kuhakikisha barabara za mitaa zinapitika kipindi chote sambamba na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii hususani kuzifikia huduma za afya, elimu kwa urahisi.
Mstahiki Meya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa akizungumza na Mwananchi Digital Ofisini kwake Leo Jumanne Mei 12, 2026. Picha na Hawa Mathias
Mbali na maboresho ya barabara za mitaa kwa mwaka 2026/27, amesema kuna mikakati ya kutenga bajeti kwa ajili ya kununua mtambo wa kushindilia barabara.
“Tutaendelea kuboresha miradi ya maendeleo, lakini katika maboresho ya barabara za mitaa halmashauri itatenga bajeti za mafuta kwa ajili ya kuwezesha mitambo hiyo kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Issa amesema wametenga zaidi ya Sh1.1 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la utawala katika halmashauri mpya ya Uyole.
“Tunatarajia kusaini mkataba kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala halmashauri mpya ya Uyole na mkandarasi ameshapatikana wakati wowote kazi itaanza,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi, Diwani wa Ilomba, Noah Mwakisu amesema kununuliwa kwa mtambo huo kutasaidia kurekebisha maeneo yanayoathiriwa na mvua.
“Tumerejesha mawasilino kwa wananchi hali ilikuwa mbaya hususani Mtaa wa Nsongwe Juu kwenda Ituha,” amesema.
Susan Michael ni mkazi wa Ituha, amesema wameona kazi inayofanywa na halmashauri, huku wakiomba kuangalia uchimbaji wa mifereji ya kupitisha maji ya mvua.
“Huku kuna maeneo msimu wa mvua wananchi wanatamani kukimbia makazi hali inakuwa mbaya na kibaya zaidi kukosekana mitalo ya kupitisha maji,” amesema.