Dar es Salaam. Takwimu mpya zilizotolewa na Serikali kuhusu ongezeko la watu wenye msongo wa mawazo zimeibua tena mjadala wa afya ya akili nchini, huku wataalamu wakieleza kuwa hali hiyo inachochewa zaidi na changamoto za kiuchumi, mabadiliko ya kijamii na kudhoofika kwa mifumo ya msaada wa kijamii.

Akizungumza bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27 juzi, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa alisema kati ya watu 1,709 waliopimwa kwa magonjwa ya afya ya akili kati ya Julai 2025 na Machi 2026, 1,362 walibainika kuwa na dalili za msongo wa mawazo na kuanza matibabu.

Kwa mujibu wa waziri huyo, takwimu hizo zimepatikana kupitia huduma za uhamasishaji na uchunguzi wa afya ya akili zinazotolewa na Serikali kwa jamii, ikiwa na lengo la kubaini mapema wagonjwa na kuwapatia matibabu.

Mchengerwa alisema Serikali pia imeendelea kuimarisha huduma za afya ya akili kupitia mafunzo kwa wataalamu na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

“Wahudumu wa afya ya jamii 50 pamoja na wataalamu 10 wa afya, walipatiwa mafunzo maalumu ya kuwasaidia kutambua na kutoa huduma kwa watu wenye changamoto za msongo wa mawazo katika maeneo yao,” alisema Mchengerwa.

Aidha, alisema kampeni za uelimishaji jamii kuhusu magonjwa ya akili kama kifafa na tawahudi, zimeendelea kutolewa kupitia maadhimisho na majukwaa ya umma, ambapo mamia ya wananchi yamefikiwa.

Mlipuko wa kimya kimya

Wataalamu wa afya ya akili na wanasaikolojia wamesema Tanzania huenda inakabiliwa na mlipuko wa kimya kimya wa matatizo ya afya ya akili unaoathiri watu wa rika mbalimbali, hususan vijana na wakazi wa mijini.

Mhadhiri wa sosholojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Faudhia Mfaume akizungumzia hilo leo Jumanne Mei 12, 2026, amesema ongezeko la matukio ya msongo wa mawazo linachochewa na shinikizo la kiuchumi na mabadiliko ya kijamii.

“Watu wengi wanapitia changamoto za maisha ya kila siku, wakibeba majukumu ya kifamilia na matarajio ya kijamii kwa wakati mmoja. Hali hii inaleta uchovu wa kihisia unaoweza kupelekea msongo wa mawazo,” amesema.

Ameongeza kuwa miji kukua kwa kasi kumeathiri pia mifumo ya msaada wa kijamii ambayo zamani ilikuwa nguzo muhimu ya kusaidia watu kukabiliana na changamoto za maisha.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Alfani Mduge amesema ukosefu wa ajira kwa vijana ni chanzo kikubwa cha msongo wa mawazo nchini.

“Wahitimu wengi hukaa muda mrefu bila ajira au wanafanya kazi zisizo na uhakika. Hii inaleta kukata tamaa na msongo wa mawazo,” amesema.

Kwa upande wake Linah Kabula, mhadhiri mwingine wa SAUT, amesema matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii pia yanachangia kuongezeka kwa matatizo ya afya ya akili.

“Watu wengi wanajilinganisha na maisha wanayoyaona mitandaoni, hali inayowafanya wajihisi hawajafanikiwa au hawatoshi,” amesema.

Dalili zinapuuzwa

Daktari bingwa wa saikolojia kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando, Kelvin Kiberiti amesema msongo wa mawazo wa muda mrefu usiopata tiba unaweza kuathiri utendaji kazi wa ubongo na hali ya kihisia.

“Watu wengi hupuuza dalili za awali kama huzuni ya muda mrefu, uchovu na kujitenga na jamii,” amesema.

Hivyo, amesisitiza haja ya huduma za afya ya akili kusogezwa karibu zaidi na wananchi kupitia vituo vya afya vya ngazi za chini.

Kwa mtazamo mwingine, matumizi ya pombe, madeni na migogoro ya kifamilia ni miongoni mwa sababu zinazoongeza visa vya msongo wa mawazo, kwa mujibu wa Isaac Lema, daktari wa saikolojia kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Magonjwa mengi ya afya ya akili tunayoyaona sasa yanahusiana na matumizi ya dawa za kulevya, pombe na msongo wa kifedha,” alisema Dk Lema.

Hatua za haraka

Wataalamu hao wamesema ipo haja ya kuimarisha elimu ya afya ya akili shuleni, vyuoni na maeneo ya kazi ili kupunguza unyanyapaa unaowazuia watu wengi kutafuta msaada.

Aidha, wameitaka Serikali kuongeza idadi ya wataalamu wa afya ya akili pamoja na kuingiza huduma hizo kwenye mfumo wa kawaida wa huduma za afya.

Watalaamu hao wanasema bila hatua za haraka, msongo wa mawazo unaweza kuendelea kuongezeka na kuwa changamoto kubwa ya afya ya umma nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *