Kilwa. Wakulima wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi wameiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Mazao Mchanganyiko (COPRA) kuongeza kiasi cha mbegu bora za ufuta katika msimu ujao wa kilimo kutokana na ubora wa mbegu zilizotolewa mwaka huu.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Mei 12, 2026, wakulima hao walisema mbegu walizopewa zimeonyesha matokeo mazuri mashambani na zina matarajio ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo. Hata hivyo, wameiomba mamlaka hiyo kuhakikisha mbegu zinawafikia mapema ili ziendane na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mkulima wa kijiji cha Pande, Hamis Juma, amesema mbegu zilizotolewa na COPRA ni bora na zina matumaini ya kuwapatia mavuno mengi msimu huu.
Wakulima wa Wilaya ya Kilwa wakimsikiliza Ofisa Kilimo wa Copra, Dorothy Mushi (hayupo pichani), alipokuwa akitoa elimu kuhusu utunzaji bora wa zao la ufuta ili kudumisha ubora wake kabla ya kupelekwa maghalani. Picha na Bahati Mwatesa
Amesema changamoto kubwa waliyoikabili ni kuchelewa kwa mbegu kufika kwa wakati huku mvua zikianza mapema mwezi Machi, jambo lililoathiri baadhi ya maeneo ya uzalishaji.
Kwa mujibu wa Juma, mvua kubwa zilizonyesha katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Lindi zimesababisha mashamba mengine ya ufuta kuathirika, hasa mazao yaliyokuwa yamefikia hatua ya kuzaa.
“Tunawashukuru COPRA kwa kutupatia mbegu bora za ufuta, lakini msimu ujao tunaomba watuwahishie mbegu ili tuweze kuendana vizuri na hali ya hewa,” amesema Juma.
Naye mkulima mwingine kutoka Kiranjelanje, Mariamu Saidi, amesema mbegu zilizotolewa zimekuwa na manufaa kwa wakulima na kuomba mamlaka hiyo kuongeza msaada wa pembejeo nyingine za kilimo, ikiwemo mbegu za mahindi.
Dorothy Mushi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mazao Mchanganyiko (COPRA), akizungumza na wakulima kuhusu utunzaji bora wa zao la ufuta ili kuhifadhi ubora wake kabla ya kupelekwa maghalani. Picha na Bahati Mwatesa
“COPRA wamefanya jambo jema sana kwa kutuletea mbegu za ufuta. Tunaomba pia watuletee na mbegu za mahindi ili kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji,” amesema Mariamu.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Kilwa, Isaya Mwakabwaga, ameishukuru COPRA kwa kutoa tani tatu za mbegu za ufuta zilizogawiwa kwa zaidi ya wakulima 2,000 wilayani humo.
Amesema Kilwa ni miongoni mwa wilaya zinazozalisha kwa wingi zao la ufuta, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza kiasi cha mbegu kinachotolewa kwa wakulima katika msimu ujao.
“Tunawashukuru sana COPRA kwa kutupatia mbegu bora za ufuta. Tunaomba msimu ujao watupatie mbegu nyingi zaidi kwa sababu Kilwa ni moja ya maeneo yanayolima ufuta kwa kiwango kikubwa,” amesema Mwakabwaga.
Naye Ofisa Kilimo kutoka COPRA, Dorothy Mushi amewataka wakulima kuzingatia ubora wa mazao yao ili kuongeza ushindani wa bidhaa hiyo sokoni.
Amesema mamlaka hiyo imefika Kilwa kutoa elimu kuhusu namna bora ya kuandaa na kuhifadhi ufuta, ikiwemo kuhakikisha unakaushwa vizuri na kuwa safi kabla ya kuuzwa.
“Tumefika Kilwa kutoa elimu kuhusu namna ya kuandaa ufuta na kuhakikisha unakuwa safi ili wakulima waweze kupata bei nzuri sokoni, hasa katika kipindi hiki ambacho ushindani wa soko umeongezeka,” amesema Mushi.