
Dar/mikoani. Ni maumivu kwa wananchi. Hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya bei ya gesi ya kupikia kupanda katika maeneo mbalimbali nchini, hali inayozidi kuongeza mzigo wa gharama za maisha.
Hali hiyo imeshuhudiwa kuanzia leo, Machi 12, 2026 baada ya mawakala wa gesi ya majumbani (LPG) kuanza kuuza bidhaa hiyo kwa bei mpya kwa watumiaji wa mwisho, huku wananchi wakilalamikia ongezeko hilo na kuonya kuwa linaweza kuwalazimisha kurejea kutumia kuni na mkaa.
Awali, tangazo lililosambaa mitandaoni leo limeonesha kuwa kuna mabadiliko ya bei za gesi likihusisha Kampuni ya Oryx Energies, hatua iliyodaiwa kuchochewa na kupanda kwa bei ya gesi katika soko la dunia kwa takriban asilimia 48.
Kwa mujibu wa tangazo hilo lililozua mjadala, bei ya mtungi wa kilo sita imeonekana kupanda kutoka Sh24,000 hadi Sh28,000, kilo 15 kutoka Sh58,000 hadi Sh63,000, na kilo 38 kufikia Sh145,000 kwa mlaji wa mwisho. Kwa upande wa mawakala, imedaiwa kuwa kilo sita imefika Sh25,500 na kilo 15 Sh57,000. Mbali na tangazo hilo lililosambaa mitandaoni, Mwananchi imepata ujumbe uliotumwa kwa mawakala kupitia barua pepe kuhusu ongezeko hilo la bei kuanzia leo.
“Tunapenda kuwataarifu rasmi kubadilika kwa bei zetu za gesi Tanzania kwa ujazo tofauti. Mabadiliko haya ni kufuatia upandaji wa bei katika soko la dunia kwa takriban asilimia 48, ambayo ni sawa na ongezeko la Sh682 kwa kilogramu.
“Pia, ongezeko la usafirishaji kwa asilimia 15 kufuatia ongezeko la mafuta, pamoja na gharama nyingine za pesa za kigeni na ongezeko la gharama za wafanyakazi kwa kampuni za kigeni,” umesomeka ujumbe huo na kuongeza:
“Pamoja na gharama zilizoongezeka kuwa juu sana, bado kampuni ya Oryx imeongeza bei kwa kiwango cha chini sana ambacho tunaamini kinahimilika kwa wateja wetu na kufanya matumizi ya nishati safi yaendelee bila kutetereka. “Tunatambua mchango wa wasambazaji wetu wakuu katika kufikisha ujumbe kwa wasambazaji wadogo kwa utaratibu mzuri bila kuleta taharuki sokoni na kwa watumiaji wa mwisho.”
Katika hitimisho la ujumbe huo imeelezwa kuwa bei zimeongezeka kwa Sh3,000 kwa mtungi wa kilogramu sita, Sh4,000 kwa mtungi wa kilogramu 15 na Sh12,000 kwa mtungi wa kilogramu 38.
“Hivyo, bei ya mtumiaji wa mwisho (Dar & Pwani) ni Sh27,000 kwa gesi ya kilogramu sita, Sh62,000 kwa mtungi wa gesi wa kilogramu 15 na Sh124,000 kwa kilogramu 38.”
Mwananchi imezungumza na mawakala mbalimbali ambao wamesema wamepokea bidhaa kwa bei mpya na hivyo kulazimika kurekebisha bei kwa watumiaji wa mwisho.
Mmoja wa mawakala wa Mkuranga mkoani Pwani (hakupenda kutaja jina) amesema alielekezwa kuwa gesi imepanda bei na hivyo kubadilisha viwango vya mauzo.
“Walipokuja jana waliniambia wanabadilisha kwa mara ya mwisho kwa bei ya zamani. Kuanzia leo (jana) bei ni mpya. Oryx ndogo ilikuwa Sh24,000 sasa ni Sh27,000, wakati mtungi mkubwa ulikuwa Sh58,000 sasa Sh62,000,” amesema.
“Total ndogo ilikuwa Sh21,000 imepanda hadi Sh24,000, na ile kubwa ya kilo 15 kutoka Sh50,000 sasa Sh55,000,” ameongeza.
Wakala mwingine anayefanya shughuli zake Mbezi (jina linahifadhiwa) amesema naye alipokea taarifa kutoka kwa msambazaji wake.
“Nimewasiliana na wakala mkuu ninakochukua mzigo, ameniambia gesi ya Oryx imepanda kuanzia leo tarehe 12. Mtungi mkubwa uliokuwa Sh58,000 sasa ni Sh62,000, maana kutoka kwake tutanunua Sh57,000,” amesema.
Isaya Antony ambaye ni wakala mkoani Arusha alisema leo asubuhi wamepewa matangazo ya bei mpya na kuwa hali hiyo imekuwa changamoto kwao na kwa wateja wao kwa ujumla.
“Mimi gesi za kampuni za Oryx na Manjis nilikuwa nauza bei moja. Gesi za kilo 15 nilikuwa nauza Sh55,000, kwa sasa nauza Sh61,000. Zile za kilo sita nilikuwa nauza Sh22,000 ila kuanzia leo nauza Sh26,000.”
Kauli ya wananchi
Hali hiyo imeanza kuibua malalamiko kutoka kwa wananchi wanaosema ongezeko hilo linaongeza mzigo wa maisha na linaweza kuathiri matumizi ya nishati safi.
“Mambo yanazidi kuwa magumu kila siku. Sasa hata gesi ambayo tulidhani ni nafuu nayo inazidi kupanda. Wakati mwingine tunalazimika kurudi kutumia mkaa,” amesema Rehema Juma, mkazi wa Temeke, jijini Dar es Salaam.
Mary Julius, mkazi wa Moshono mkoani Arusha, amesema hali ya kupanda kwa bei ya gesi inaenda kinyume na juhudi za Taifa za kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
“Serikali inatuhamasisha tutumie gesi ili kulinda mazingira, lakini bei inapanda ghafla. Hii inakuwa vigumu kwa familia nyingi kuendelea kuitumia,” amesema.
Kwa upande wake, Abdilah Kassim, mkazi wa Arusha amesema ongezeko la bei limekuwa mzigo mkubwa kwa kaya nyingi za kipato cha chini na kuwa wengi watalazimika kurudi kwenye matumizi ya kuni na mkaa ili kudhibiti gharama.
“Sisi tunataka kutumia gesi kama nishati safi, lakini bei inapopanda kila wakati inatufanya turudi kwenye mkaa au kuni. Hii ni changamoto kubwa sana kwa wananchi wa kawaida,” amesema.
Amesema kupanda kwa gharama hizo kutasababisha ongezeko la uharibifu mkubwa wa mazingira na kuiomba Serikali kuangalia namna ya kudhibiti upandaji wa bei kwa bidhaa muhimu kama gesi.
Hali ilivyo mikoani
Mkoani Simiyu, bei ya gesi ya Kampuni ya Oryx Energies imepanda ambapo mtungi wa kilo 15 sasa utajazwa kwa Sh63,000, kilo sita ni Sh28,000 huku kilo 38 ikiwa Sh145,000. Kwa upande wa Taifa Gas na Mihan Gas bado wanaendelea na bei za zamani.
Mikoa ya Mwanza na Mbeya kampuni nyingi hazijapandisha bei.
Wakati sintofahamu hiyo ikiendelea, Meneja wa Masoko wa Oryx Energies, Peter Ndomba, amekanusha taarifa hizo akisema hakuna mabadiliko rasmi ya bei yaliyotangazwa na kampuni.
“Hakuna taarifa yoyote ya kupanda kwa bei za gesi. Sijui hizo taarifa zimetoka wapi. Kama kungekuwa na mabadiliko, lazima kungekuwa na mawasiliano rasmi. Itabidi tuwatafute hao mawakala waliopandisha bei,” amesema Ndomba.
Kauli kama hiyo pia imetolewa na ofisa kutoka Kampuni ya Total Gas ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msemaji, akisisitiza kuwa kampuni yao haijapandisha bei za gesi kwa sasa.
Mwananchi imemtafuta Meneja wa Masoko na Mauzo wa Oryx, Shaban Fundi, kutolea ufafanuzi ujumbe huo na mabadiliko hayo ya bei. Amejibu, “Ngoja nifuatilie nipate taarifa ya kina, nitakurudia.” Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni meneja huyo hakurejea kutoa majibu na juhudi za kumtafuta hazikuzaa matunda.
Wakati hali ikiwa hivyo, Aprili 3, 2026, Kampuni ya Taifa Gas ilitangaza kuwa haitapandisha bei ya gesi ya majumbani (LPG), licha ya kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la kimataifa.
Meneja Mkuu wa Taifa Gas, Devis Deogratius, alipozungumza na waandishi wa habari alisema ongezeko la bei katika soko la kimataifa limeongeza gharama za ununuzi na usambazaji wa gesi, lakini kampuni imechukua hatua ya kubeba mzigo huo ili kuwasaidia wateja wake.
Ewura yafuatilia soko
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Gerald Maganga, amesema gesi ya kupikia ni nishati muhimu na mamlaka hiyo inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za kimataifa na za ndani.
Amesema lengo ni kuhakikisha hakuna utozaji wa bei za juu kupita kiasi na kulinda mlaji pamoja na kuhakikisha soko linabaki la haki na lenye ushindani.
“Ewura hufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa bei za LPG katika soko la kimataifa na kuzilinganisha na soko la ndani ili kuhakikisha watumiaji wanalindwa dhidi ya bei zisizo za haki, huku pia tukihakikisha mazingira ya soko yanabaki kuwa endelevu na yenye ushindani kwa wazabuni,” amesema Maganga.
Imeandikwa na Elizabeth Edward (Dar es Salaam), Janeth Mushi (Arusha), Saddam Sadick (Mbeya), PraiseGod Mgumba (Mwanza) na Samwel Mwanga (Simiyu).