Lisbon, Ureno. Hatima ya kocha Jose Mourinho kurejea tena Santiago Bernabeu kuinoa Real Madrid, imeendelea kuwa fumbo baada ya kukwepa kujibu hilo alipokutana na waandishi wa habari jana.

Mourinho anatajwa kurejea Real Madrid baada ya miaka 13 alipoondoka ndani ya klabu hiyo, huku taarifa zikidai kuwa yupo kwenye mazungumzo ya mwisho yanayoendelea kati yake na mabosi wa klabu hiyo ya Hispania.

“Kuna mechi dhidi ya Estoril, na kuanzia Jumatatu nitaweza kujibu maswali kuhusu mustakabali wangu na Benfica,” amesema Mourinho.

Kocha huyo raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 63 ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba ya ukocha wa timu hiyo.

Inaelezwa kuwa Madrid inaweza kumpata Mourinho kwa ada ya paundi 2.6 milioni (Sh9 bilioni) pekee endapo itakamilisha dili hilo ndani ya siku 10 baada ya mchezo wa mwisho wa Benfica msimu huu dhidi ya Estoril utakaochezwa Mei 16.

Taarifa kutoka Hispania zinaeleza kuwa rais wa Madrid, Florentino Pérez, tayari ameanza mazungumzo binafsi na Mourinho kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Álvaro Arbeloa mwishoni mwa msimu huu.

Meneja wa Benfica, Jose Mourinho (kulia), akiwa na nyota wa zamani wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo (kushoto) wakati wawili hao walipokuwa wakihudumu Santiago Bernabeu. Picha na Mtandao

Katika kipindi chake cha kwanza Santiago Bernabéu, Mourinho aliipa Madrid ubingwa wa La Liga, Copa del Rey na Spanish Super Cup, huku akionyesha ushindani mkubwa dhidi ya Barcelona iliyokuwa chini ya Pep Guardiola.

Ripoti hizo zinaeleza kwamba Mourinho anaamini bado ana kazi ambayo hajamaliza Madrid, hasa baada ya kushindwa kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo alipokuwa kocha wa timu hiyo.

Meneja wa Benfica, Jose Mourinho amesema atajibu kuhusu hatma ya kurejea Real Madrid siku ya Jumatatu Mei 18, 2026 baada ya mchezo wa mwisho wa Benfica. Picha na Mtandao

Pia imeelezwa kuwa kocha huyo mwenye miaka 63 yupo tayari kukataa ofa kutoka Chelsea kwa ajili ya kurejea Hispania.

Mourinho kwa sasa anaelekea kumaliza msimu bila kupoteza mchezo wowote akiwa Benfica, jambo lililomfanya kuwa chaguo namba moja kwa mabosi wa Madrid licha ya kuwa aliwahi kuinoa klabu hiyo mwaka 2010 hadi 2013.

Madrid inatajwa kutaka kumtambulisha Mourinho rasmi kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia huku mazungumzo yakitarajiwa kushika kasi mara baada ya msimu wa ligi kumalizika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *