Nigeria. Moja ya tukio ambalo liligonga vichwa vya habari ni kuhusu, ubunifu na mitindo iliyoonekana katika usiku wa ugawaji wa Tuzo za ‘Africa Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCA)’ zilizofanyika jijini Lagos, Nigeria.
Katika usiku huo mfanyabiashara na mwanamitandao maarufu Queen Mercy Atang, aliwavutia wengi baada ya kuvalia gauni linalodaiwa kutengenezwa kwa kutumia takribani mikate 500.
Inaelezwa kuwa, Queen ambaye alipata umaarufu baada ya kushiriki katika msimu wa sita wa ‘Big Brother Naija’ mwaka 2021. Alitumia mwonekano huo wa kipekee kuitangaza biashara yake ya mikate na keki inayojulikana kama ‘Swit Cakes & Desserts’.
Akizungumza na BBC katika hafla hiyo Queen alieleza, hakukuwa na sehemu bora zaidi ya kuitangaza biashara yake kuliko jukwaa la AMVCA. “Nilifikiria sana nitaitangaza wapi biashara yangu, lakini akili ikaniambia nikatangaze wapi kwengine, biashara yangu kama si hapa AMVCA,”alisema Queen
Video zilizosambaa mitandaoni zilimuonyesha akitembea kwenye zulia jekundu huku wasaidizi wake wakimsaidia kubeba sehemu ya chini ya gauni hilo kubwa ambalo lilifunikwa kwa mikate.
Kufuatia na mwonekano huo baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii walitoa maoni yao. Wachache wakimpongeza kwa ubunifu wake wa kutangaza biashara. Huku wengi wakimkosoa na kuhoji kuhusiana na matumizi ya chakula katika mavazi wakati asilimia kubwa ya watu duniani wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula.
Hatahivyo Queen alimshukuru mbunifu wake kwa kufanikisha wazo hilo. Gauni hilo limebuniwa na mbunifu maarufu Toyin Lawani ‘Tiannah’s Empire’.
“Toyin, asante kwa ubunifu wako na kwa kusaidia kuitangaza brand yangu. Nilichotaka ni gauni litakaloonyesha kuwa nina biashara ya bakery, na umefanikisha hilo. Mwanzoni nilikuwa na hofu, lakini uliendelea kunitia moyo hadi mwisho,” alisema Queen