
Miongoni mwa mada kuu zinazozungumzwa nchini hivi sasa ni mwelekeo wa hali ya kisiasa Zanzibar, hasa katika jitihada za kuondoa mvutano uliotokana na uchaguzi mkuu wa Zanzibar.
Uchaguzi huo ulifanyika Oktoba 29, mwaka jana ambao Chama cha ACT-Wazalendo kinadai haukuwa huru na haki.
Katika harakati za kutafuta maridhiano, kuimarisha umoja na kuondoa uhasama wa kisiasa, tena zinasikika taarifa za kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, kumekuwa na tetesi na baadaye taarifa rasmi kuhusu mazungumzo ya kuunda SUK mpya. Miongoni mwa watu wanaohusika katika juhudi hizo ni marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Ali Mohammed Shein.
Iwapo maelewano yatafikiwa, itakuwa ni mara ya nne kwa Zanzibar kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hata hivyo, uzoefu wa vipindi vitatu vilivyopita unaonyesha kuwa mfumo huo umekuwa wa kusuasua na mara nyingi huvurugika uchaguzi unapokaribia.
Kilichoonekana wazi ni kwamba SUK imekuwa ikitumika zaidi kama njia ya kupunguza joto la kisiasa kuliko kujenga msingi wa maridhiano ya kudumu. Kwa muda wote, CCM na ACT-Wazalendo wamekuwa wakitupiana lawama kuhusu sababu za kutokuwapo kwa maelewano yenye tija. Ikiwa kweli ipo nia safi ya kutafuta suluhu ya kudumu kwa maslahi ya Zanzibar na wananchi wake, si busara kupuuza ukweli kwamba chaguzi nyingi zilizofanyika Zanzibar zimekuwa zikikumbwa na dosari mbalimbali.
Ndiyo maana baadhi ya waangalizi wa ndani na nje ya nchi wamekuwa wakisita kuziita chaguzi hizo kuwa huru na za haki.
Miongoni mwa mambo yaliyotia shaka ni namna ya ugawaji wa majimbo, uendeshaji wa uandikishaji wa wapigakura, pamoja na madai ya maelfu ya wananchi kunyimwa haki yao ya kupiga kura.
Pia, kumekuwa na malalamiko kuhusu kuwapo kwa majina ya watu walioandikishwa zaidi ya mara moja katika maeneo tofauti, majina ya watu waliofariki dunia kuendelea kuwamo katika daftari la wapigakura, pamoja na idadi ya kura kuzidi idadi ya wapigakura walioandikishwa. Aidha, zilisambaa picha na kanda za video zikionyesha watoto wasiokuwa na umri wa kupiga kura wakidaiwa kushiriki uchaguzi wakiwa wamevaa sare za vikosi vya ulinzi vya Zanzibar.
Kulikuwa pia na video zilizowaonyesha baadhi ya watendaji wa uchaguzi wakipiga kura kwa namna iliyozua maswali mengi kutoka kwa wananchi.
Jambo jingine lisilopaswa kufumbiwa macho ni matokeo ya uchaguzi kuonyesha ACT-Wazalendo kutoshinda hata jimbo au wadi moja katika uchaguzi wa madiwani na Baraza la Wawakilishi, hata katika maeneo yanayotajwa kuwa ngome zao za kisiasa zilizokuwa zikiwapa ushindi mkubwa katika chaguzi zilizopita.
Kwa sasa mazungumzo yanaendelea na tunaambiwa yamefikia hatua nzuri. Ni matumaini ya wengi kwamba mwafaka utapatikana ili wananchi warejee katika hali ya kuaminiana, kupendana na kuishi kwa mshikamano kama ilivyokuwa zamani.
Hata hivyo, ni muhimu dosari zote zilizo wazi na zile zilizojificha zipewe uzito unaostahili na kutafutiwa suluhisho la kudumu.
Miongoni mwa mambo yanayohitaji kuangaliwa kwa makini ni suala la kura ya mapema, ambalo umuhimu wake umeendelea kuzua mijadala na mashaka kutoka kwa baadhi ya wadau wa kisiasa.
Vilevile, muundo wa SUK usibaki katika ngazi za juu za uongozi pekee, bali ushuke hadi katika ngazi za majimbo, wilaya na shehia ili kuimarisha ushirikishwaji na kuondoa hisia za kutengwa kisiasa.
Wakati kukiwa na mjadala wa kuundwa tena kwa SUK, zimeibuka pia kauli kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa wanaopendekeza Katiba ya Zanzibar iwekwe pembeni ili Rais Dk Hussein Mwinyi aendelee kuongoza hata baada ya kumaliza muhula wake wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa Katiba.
Baadhi yao wamefika mbali zaidi kwa kudai kuwa Dk Mwinyi anapaswa kuwa rais wa maisha, huku wanaosisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa Katiba wakitajwa kuwa si wenzetu, au kwamba hawaitakii mema Zanzibar.
Swali la msingi linabaki kuwa: ni nani asiyeitakia mema Zanzibar? Je, ni wale wanaotaka Katiba iheshimiwe, au wale wanaotaka iwekwe pembeni?
Historia inaonyesha si mara ya kwanza kwa mawazo ya aina hiyo kujitokeza. Katika miaka ya nyuma, walikuwapo waliotaka marais wastaafu akiwamo Salmin Amour Juma, Amani Abeid Karume na Ali Mohammed Shein kuendelea kuongoza hata baada ya mihula yao ya kikatiba kumalizika. Hata hivyo, juhudi hizo ziligonga mwamba na Katiba ikaendelea kuheshimiwa.
Sasa tena sauti hizo zimerudi. Wapo hata wanaofanya mzaha wakisema kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, wabunge, wawakilishi na madiwani nao wawe viongozi wa maisha. Hili ni jambo la hatari kwa mustakabali wa demokrasia na utawala wa sheria.
Kutaka Rais Mwinyi awe rais wa maisha ni sawa na kusema hakuna tena haja ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa wala uchaguzi Zanzibar. Ni vyema masuala yote haya yakazingatiwa kwa umakini ili Zanzibar ipate maridhiano ya kweli na ya kudumu, badala ya suluhu za muda ambazo huibua migogoro kila uchaguzi unapokaribia.
Tuombe Mungu mazungumzo ya kuunda SUK ya nne yafanikiwe, amani iliyopo Zanzibar iendelee kudumu.