
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anakabiliwa na upinzani mkali baada ya kukatiza kikao cha mjadala katika kongamano la Africa Forward Summit nchini Kenya akiwataka hadhirina wanyamaze kimya.
Macron alivamia jukwaani kuwakemea watazamaji kwa kile alichokiita “ukosefu wa heshima kabisa,” akiwashutumu kwa kuvuruga wazungumzaji wakati wa onyesho la wasanii na wajasiriamali wachanga. Hapo awali Macron alikuwa amejitambulisha kama “muungaji mkono wa Pan-Africa” wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Mkutano wa Afrika na Ufaransa mjini Nairobi ulilenga kuonyesha sera mpya ya Ufaransa kwa bara hilo ikiwa ni— mabadiliko kutoka utawala wa zamani wa wazi wa kikoloni hadi kile ambacho Paris inakielezea kama ushirikiano wa usawa.
Video za uingiliaji kati mkali wa Macron siku ya Jumatatu zilisambaa haraka kwenye mitandao ya kijamii na kuzibua mchanganyiko wa hisia za kejeli, sifa na ukosoaji.
Akionekana kukerwa na kelele zilizokuwa ukumbini, Macron alipanda ghafla jukwaani na kumuomba mzungumzaji amkabidhi kipaza sauti, akisema “atarejesha utulivu.”
Akihutubia hadhira kwa Kiingereza, Rais wa Ufaransa aliwakosoa waliohudhuria kwa kukatiza wazungumzaji na kusababisha usumbufu kwenye kikao hicho.
Baadhi ya hadhirina walipongeza hatua yake, lakini Macron pia amekosolewa kuhusu majibu yake.
“Hebu fikiria nini kingetokea iwapo kiongozi wa nchi ya Kiafrika angefanya jambo hilohilo huko Marekani au Ulaya,” amehoji Thierno Mbaye, mwanafunzi wa historia katika chuo kikuu cha mji mkuu wa Senegal, Dakar.
“Alijifanya kama mwalimu wa shule akiwakemea watoto,” Mbaye ameiambia The Associated Press.
Uingiliaji kati huo wa Macron pia umekosolewa nchini Ufaransa.
“Mara tu anapoingia barani Afrika, hawezi kujizuia kutenda kama mkoloni,” amesema Danièle Obono, mbunge wa chama cha mrengo wa kushoto cha France Unbowed, katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Mkutano wa Afrika Forward, ambao ulimalizika jana Jumanne ulifanyika huku kukiwa na mzozo kati ya Ufaransa na makoloni yake ya zamani, hasa katika nchi za Afrika Magharibi.
Ufaransa, kwa muda mrefu, imekuwa ikitekeleza sera ya kikoloni ya kuendeleza ushawishi wa kiuchumi, kisiasa na kijeshi chini la jina la Françafrique, ambayo ilijumuisha kuwaweka maelfu ya wanajeshi katika maeneo ililoyadhibiti.
Baada ya miaka mingi ya ukosoaji kutoka kwa viongozi na vyama vya upinzani katika nchi nyingi za Afrika Magharibi kuhusu kile walichokielezea kama mbinu ya kudhalilisha na ya kinyama, Ufaransa imeondoa sehemu kubwa ya wanajeshi wake katika nchi za Magharibi mwa Afrika.
Awali, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alikabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya kujitambulisha kuwa ni ” Sisi ndio waungaji mkono halisi wa Umoja wa Afrika (Pan-Africanists).
Pan-Africanism inaashiria itikadi inayotaka umoja wa Waafrika na kufutilia mbali ukoloni. Kwa kuzingatia historia ya ukoloni wa Ufaransa kote barani Afrika, kauli hiyo imezusha mshangao na mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Umoja wa Afrika si chapa, Bw. Macron, wala si msimamo wa kidiplomasia,” alisema Farida Nabourema, mwanaharakati wa haki za binadamu wa Togo, katika barua ya wazi, siku ya Jumatatu.
Farida Nabourema ameongeza kuwa: “Pan Africanism ni falsafa ya kisiasa ambayo inapinga kila kitu ambacho Ufaransa ilitumia karne tatu ikisema ndiyo kwa utumwa, ndiyo kwa ukoloni na ukoloni mamboleo.”