Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar ameeleza katika mahojiano marefu aliyofanyiwa na televisheni ya Al Jazeera kwamba, Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uko mara zaidi hivi sasa kuliko ulivyokuwa huko nyuma.
Hamad bin Jassim Al Thani, aliwahi kuwa mfikishaji ujumbe wa Marekani kwa Iran mwishoni mwa muongo wa 1990. Katika mahojiano hayo na Aljazeera, waziri mkuu huyo wa zamani wa Qatar amesisitiza kwamba, kuishambulia kijeshi Iran haukuwa uamuzi uliochukuliwa papo kwa papo, bali ni sehemu ya ajenda ya muda mrefu ya waziri mkuu wa utawala wa kizayuni Benjamin Netanyahu ya kubadilisha ramani ya Mashariki ya Kati, yaani Asia Magharibi.
Kwa mujibu wa Hamad bin Jassim Al Thani, tangu wakati wa urais wa Bill Clinton, utawala wa Kizayuni umejaribu kutumia kila njia ili kuisukuma Marekani kwenye makabiliano ya kijeshi na Iran kwa kisingizio cha mpango wa nyuklia wa Tehran, lakini serikali zilizopita za Marekani ikiwemo hata ya muhula ya kwanza ya Trump, hazikushawishika kuanzisha vita kamili dhidi ya Iran. Tofauti ya mara hii na zilizopita ni kwamba, Netanyahu amefanikiwa kuishawishi Washington kwa kuiahidi kuwa vita hivyo vitakuwa vya “muda mfupi na vya haraka” na kwamba utawala wa Iran “utaanguka” ndani ya wiki chache tu.
Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar amelibainisha hilo kwa kusema: “Netanyahu alikuwa ameiaminisha Marekani kwamba itachukua wiki chache tu kuubadilisha mfumo wa utawala wa Iran, lakini nimeshaeleza mara kadhaa kwamba wao hawaujui muundo wa utawala ulioko nchini Iran ambao umejengwa kwa muda wa miaka 47 tangu Shah alipopinduliwa. Mfumo wa utawala wa Iran hivi sasa uko imara zaidi kuliko ulivyokuwa huko nyuma”.
Hamad bin Jassim Al Thani ameongeza kuwa, Wairan watafaidika na vita ili kustawisha uwezo wao wa kijeshi na kiteknolojia, kama inavyopasa kufanywa hivyo pia na nchi za Ghuba Uajemi. Uchambuzi wa aina hii haujafanywa na Hamad bin Jassim Al Thani peke yake. Wataalamu wengi wa kimataifa nao pia wamefikia hitimisho sawa na hilo. Ndani ya Iran kwenyewe, Ali Larijani, Katibu wa zamani aliyeuawa shahidi wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa, aliwahi kusema: “Ni hakika kwamba sisi tuko imara zaidi kuliko tulivyokuwa hapo kabla; tumejiandaa katika kipindi cha miezi saba au minane iliyopita, tumetambua na kurekebisha udhaifu wetu”.
Kwa upande mwingine, mashirika ya kiintelijensia na kijasusi ya Marekani nayo pia yameionya Washington kwamba kucheza bahati nasibu ya tamaa ya kukaribia kusambaratika mfumo wa utawala wa Iran ni kosa la kistratejia.

Ripoti ya siri ya Baraza la Taifa la Intelijensia la Marekani (NIC) ambayo ilitayarishwa kabla ya vita kuanza ilieleza bayana kwamba hata kama litafanywa shambulio kubwa la kijeshi halitaweza kuuangusha Mfumo wa utawala wa Iran, kwa sababu mfumo huo umebuni “protokoli maalumu zinazouhakikishia kubaki hata kama viongozi wake wakuu watauawa.”
Susan Maloney, mtaalamu mwandamizi wa masuala ya Iran katika Taasisi ya Brookings, ameielezea tathmini hiyo kama “uchambuzi wa kina kiuelewa kuhusu utawala wa Iran na taasisi na michakato ambayo imeanzishwa kwa miaka mingi”.
Sauti zinazofanana na hizo zimesikika pia kutoka hata kwa maafisa wa usalama wa utawala bandia wa Israel. Yaakov Amidror, mwenyekiti wa zamani wa baraza la usalama wa taifa la utawala huo wa kizayuni ametamka wazi kwamba, Iran, tofauti na nchi nyingi za eneo, ambazo yeye ameziita “bandia,” ina “muundo wa kina wa kisiasa na kiutamaduni na uliokita mizizi ya kitaasisi” na kwamba “kucheza bahati nasibu ya tamaa ya kuanguka papo hapo utawala wa Iran mara tu baada ya kupata kipigo kikubwa cha kijeshi ni tathmini potofu isiyo na msingi wa ufahamu wa hali ya huko”. Amidror amebainisha pia kuwa “eneo la Asia Magharibi linashuhudia marekebisho ya kimsingi” na kwamba si sahihi kuweka tamaa ya aina yoyote juu ya kuanguka haraka mfumo wa utawala wa Iran.
Hamad bin Jassim Al Thani, aliyekuwa waziri mkuu na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Qatar, ambaye huko nyuma aliwahi kutahadharisha juu ya hatari ya vita kupitia ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii, amebainisha pia kwamba, hatua hiyo ya kijeshi haina manufaa kwa eneo na kwamba Marekani imesababisha madhara kwa washirika wake katika Ghuba ya Uajemi kwa sababu Magharibi haizishirikishi katu na kwa dhati nchi za eneo hilo katika uchukuaji maamuzi yanayohusu mustakabali wao. Kwa mujibu wa Hamad bin Jassim Al Thani, kinachojiri hii leo si mgogoro wa kupita tu, bali ni mabadiliko ya kimkakati ambayo yataiathiri Mashariki ya Kati kwa miongo kadhaa.
Wakati huo huo, uchambuzi wa wanafikra mbalimbali unasisitiza juu ya kosa la kihistoria la kimahesabu lililofanywa, kwa kueleza kwamba, kudhani kuwa mashinikizo makubwa ya kijeshi ya wiki kadhaa tu yanaweza kuusamabaratisha muundo wa nguvu ambao umezatitiwa kwa karibu miongo mitano ni udhanifu na mawazo hewa yanayokinzana na tajiriba ya huko nyuma, kuanzia Iraq na Afghanistan hadi kwenye viitwavyo vikwazo vya kulemaza. Kwa maneno mengine, sio tu Iran haitadhoofika katika medani hii, lakini pia itanufaika na vita kwa ajili ya kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi na kiteknolojia. Huu ndio ukweli ambao afisa mkuu wa zamani wa Qatar, pamoja na wachambuzi waandamizi wa Marekani na Israel, wanautamka leo hii kinagaubaga, ya kwamba: Mfumo wa utawala wa Iran hivi sasa uko imara zaidi kuliko ulivyokuwa huko nyuma…/