
Dodoma. Bunge la Tanzania litakuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa wabunge wanawake wa nchi 12 za Jukwaa la Nchi za Maziwa Makuu katika mkutano utakaofanyika Novemba 2 hadi 5, 2026 jijini Dar es Salaam.
Jukwaa hilo linalojulikana kama ICGLR linashughulikia masuala ya amani, usalama, demokrasia, na maendeleo kwa nchi hizo ikiwemo kundi la wanawake.
Akizungumza wakati wa kutangaza mkutano huo, Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kihistoria na inajiandaa kupokea wageni na wanataka kuhakikisha mkutano unafanyika kwa ufanisi na mafanikio makubwa.
Spika amesema Tanzania itahakikisha inaandaa huduma zote za chakula, malazi kwa wageni kwani mkutano huo ni mkubwa unaobeba historia ya nchi.
Katibu wa Bunge, Baraka Leonald na Sekretariati ya Jukwaa la Maziwa Makuu kupitia Katibu wake, Dk Deo Mwapinga wametiliana saini kuhusu mkutano huo wakitaja sababu za kuuleta nchini ni kutokana na Taifa kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za wanawake.
Dk Mwapinga amesema wamechagua kuleta mkutano huo Tanzania kutokana wazo la kuanzisha sekretariati hiyo lilizaliwa Tanzania mwaka 2004 wakati wa utawala wa hayati Benjamin Mkapa.
Amesema, Tanzania imekuwa kinara wa masuala ya jinsia, ulinzi na usalama ndiyo maana sekretariati ya jukwaa hilo imeleta mkutano huo kama malengo ya jukwaa katika kupigania amani, ulinzi, uimara na maendeleo.
Takwimu za Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) zinaonyesha, Tanzania ina nafasi ya nne kwa kuwa na wanawake asilimia 38 kwenye Bunge, ikitanguliwa na Rwanda, Burundi, Angola na nchi ya mwisho kwa idadi ndogo ya wabunge wanawake ni Jamhuri ya Afrika ya Kati yenye asilimia 11 tu.
Mmoja wa wabunge wawakilishi kwenye Jukwaa hilo Ezra Chewelesa amesema, mkutano huo ni wa kihistoria kwa Tanzania na Bunge hilo ambalo wanawake ni asilimia 38.
Chiwelesa amesema, katika ukanda huu kuna migogoro mingi DRC, Sudan Kusini na Sudan, hivyo Tanzania imejipatia sifa kwa ajili ya kutetea haki za wanawake kutokana na ukweli vita inapotokea wao ndiyo waathirika wakuu, hivyo kampeni ni kuwa ukanda salama kwa kuondoa migogoro hiyo.
Jukwaa la Ukanda wa Maziwa Mkuu lina wanachama 12 na linaongozwa na sekretariati ambayo makao makuu yake yapo Kinshasa DRC, wanachama wake mbali na Tanzania ni Angola, Burundi, Jamhuri ya Kati, DRC, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Uganda na Zambia.