Arusha. Mabadiliko makubwa ya kiuongozi ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) yanatarajiwa kuanza rasmi kabla ya mwisho wa mwaka huu, baada ya kanisa hilo kueleza kuwa mchakato wa kupata katiba mpya umefikia hatua za mwisho.

Katiba hiyo mpya inatarajiwa kuondoa mfumo wa sasa unaozipa dayosisi mamlaka kamili ya kujiendesha na badala yake kuimarisha mamlaka ya uongozi mkuu wa kanisa, hatua inayotajwa kuwa suluhisho la muda mrefu katika kushughulikia migogoro na masuala ya nidhamu ndani ya dayosisi mbalimbali.

Mabadiliko hayo yanakuja baada ya wajumbe 214 kati ya 248 wa mkutano mkuu wa 21 wa KKKT uliofanyika Agosti 25, 2023, kuridhia pendekezo la kuwa na katiba moja ya kanisa, badala ya kila dayosisi kuwa na katiba yake.

Kwa mabadiliko hayo, katiba hiyo mpya inakwenda kuwa na mkuu wa kanisa mwenye mamlaka zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Kupitishwa kwa pendekezo hilo, kunamaanisha kuwa mkuu wa kanisa atakuwa na uwezo wa kuwachukulia hatua maaskofu na wachungaji wanaokiuka maadili.

Hata hivyo, mkuu wa kanisa hatafanya hivyo peke yake, bali kwa kutumia chombo cha kikatiba kitakachoundwa.

Muundo huu, imeelezwa kwamba unalenga kuwa tiba iliyotafutwa kwa muda mrefu, ya namna ya kushughulikia migogoro na nidhamu katika dayosisi mbalimbli nchini.

Katiba iliyopo inaelekeza  kila dayosisi kuwa na mamlaka kamili na vyombo vyake vyenye uamuzi, jambo lililokuwa linaleta ugumu kwa mkuu wa kanisa kuingilia pale mivutano inapotokea.

Chini ya mabadiliko hayo, taarifa ambazo mwananchi limezipata zinaeleza kuwa kila dayosisi itaendelea kuwa na askofu wake, msaidizi wake na vyombo vyake, ambavyo sasa vitaendeshwa kwa kutumia kanuni ndogo zitakazotungwa.

Katibu Mkuu wa KKKT, Rogath Mollel akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Mei 13, 2026, amesema maandalizi ya katiba hiyo yanaendelea na mkutano mkuu maalumu wa kuipitisha unatarajiwa kufanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Akizungumza Mei 10, 2026 katika ibada ya kumwingiza kazini Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Magharibi na Kati iliyofanyika katika Usharika wa Tabora Mjini, Mollel alisema kanisa limefanya tathmini ya kina kuona maeneo yenye udhaifu katika mfumo wake wa utendaji.

Amesema tathmini hiyo imeonyesha umuhimu wa kuandika upya katiba ya kanisa ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji, kuimarisha ustawi na kuhakikisha uendelevu wake wa muda mrefu.

“Kikao cha halmashauri kuu kilichokaa mwezi Aprili kimepokea taarifa kwamba sasa kazi ile imefika mahali pazuri na huenda kabla ya mwisho wa mwaka huu tutakuwa na mkutano wa katiba ili tuweze sasa kwenda kuipitisha katiba mpya,” amesema.

Mollel amesema baada ya maoni kupitishwa kwenye dayosisi zote na vituo, halmashauri kuu maalumu itakaa kwa ajili hiyo na Septemba wataitisha mkutano mkuu wa katiba.

“Tunomba sana jambo hili tuliweke katika maombi, tuombee kazi hii kubwa. Kwa sababu tunapokuwa na katiba ambayo ni imara na yenye nguvu, itatusaidia sana kuepuka migogoro lakini kwenda kwa kasi zaidi na ufanisi zaidi kama kanisa ambalo duniani ni la pili kwa ukubwa, basi na namna ya utendaji wetu idhihirike hivyo hivyo,” amesema.

Migogoro na Katiba

Hata hivyo, akizungumzia mabadiliko hayo, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amesema katiba haitamaliza migogoro moja kwa moja, lakini itasaidia uongozi kuwa na nyenzo bora za kushughulikia changamoto hizo kwa wakati na kwa ufanisi zaidi.

Amesema migogoro hailetwi na katiba, bali ni sehemu ya ukuaji wa kanisa.

 “Migogoro  ni changamoto kwa uongozi kujifunza mbinu za kuitatua, kwa hiyo mtu asije akakaa akasema eti katiba moja ndiyo itakayomaliza migogoro, hakuna migogoro itakayokwisha kwa kumalizwa na katiba, katiba inasaidia uongozi  kukabiliana na migogoro inapojitokeza,” amesema Askofu Bagonza.

Amesema: “Tangu Kanisa la kwanza la Bwana Yesu migogoro imekuwepo. Migogoro hailetwi na katiba na wala haitaondolewa na Katiba, lakini katiba inasaidia uongozi kukabiliana nayo inapojitokeza,” amesema Askofu Bagonza.

Ameongeza kuwa kazi iliyofanywa na kamati ya katiba ilikuwa ni kukusanya maoni kutoka dayosisi zote 28 kwa lengo la kuboresha mfumo wa sasa wa uongozi na utendaji wa kanisa.

Awali 2023

Awali akitangaza uamuzi huo Agosti 25, 2023 mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Makumira mkoani Arusha, Mkuu wa Kanisa hilo aliyemaliza muda wake, Askofu Fredrick Shoo alisema asilimia 86 ya wajumbe waliridhia pendekezo hilo.

Dk Shoo, ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, alisema idadi ya wapigakura ilipaswa kuwa 252, ila waliokuwepo ni 248 na kati yao, 214 walipiga kura za Ndiyo, sawa na asilimia 86 na za Hapana zilikuwa 36, sawa na asilimia 14.

“Hakuna kura iliyoharibika na hili nalifurahia sana, asanteni sana. Inaonyesha ukomavu wa wajumbe na kwa maana hiyo basi patano letu limepita kwamba KKKT tuwe na katiba moja kwa asilimia 86 ambazo ni zaidi ya theluthi mbili,” alisema.

Waunga mkono mabadiliko

Akizungumza baada ya uamuzi huo, Mwanasheria wa KKKT, Azaeli Mweteni amesema katiba moja iliyoridhiwa na wajumbe, itaondoa katiba za dayosisi.

“Kisheria ni kwamba mkutano mkuu wa 21 wa KKKT umepitisha mchakato wa katiba moja ya kanisa kwa sababu lililetwa pendekezo la kuandaa katiba moja ambayo itaziondoa nyingine za dayosisi na kuwa na moja,” amesema Mweteni.

Amesema katiba hiyo mpya inalenga kuliongezea nguvu kanisa ili liendelee kuwa moja kama ilivyokusudiwa.

“Hii italeta mabadiliko ya kiutendaji, lakini pia kuimarisha mfumo wa kiutawala, mfumo wa kiuongozi katika kanisa na kuendelea kuimarisha kanisa kuwa moja na kuimarisha uwajibikaji ndani ya kanisa,” amefafanua.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo kutoka Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Aneth Mnzava amesema kanisa kuwa na katiba moja kutasaidia kutekeleza dhana ya umoja na litakuwa na nguvu zaidi kuliko ilivyo sasa.

“Kanisa ni uwakilishi wa Mungu hapa duniani, umoja wetu wa kanisa ndiyo ishara ya anachotaka Mungu, kuwa na katiba moja kunatekeleza kwa vitendo dhana ya umoja kwa jinsi tulivvo sasa,” amesema na kuongeza: “Wanaofuatilia historia ya KKKT wanafahamu kwamba tulianza na makanisa saba, tukawa na dayosisi saba na kila dayosisi ilikuwa na nguvu yake, ila tunaona kule juu kunatakiwa kuwe na nguvu zaidi.”

Amesema watakapokuwa na katiba moja itawapa nafasi na fursa ya kusema KKKT kuanzia juu ni wamoja na katika dayosisi zao, ni watekelezaji wa moja kwa moja wa maelekezo yanayotoka juu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *