Mirerani. Wafanyabiashara wadogo 100 wa madini wenye leseni (mabroka) wameshiriki kwenye mnada wa madini ya vito Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Ofisa madini mkazi (RMO) Mirerani, George Kaseza akizungumza leo Jumatano Mei 13, 2026 amesema wafanyabiashara hao 100 wamejiandikisha kushiriki mnada huo unaofanyika katika jengo la soko la madini Mirerani.

Kaseza ameeleza kwamba wafanyabiashara hao wanashiriki mnada huo kwa kujisajili na kutoa bei yao kwa njia ya mtandao baada ya kukagua madini hayo kwa uwazi.

Amesema wafanyabiashara hao wadogo wote wamepewa fursa ya kushiriki bila kuzuiwa ili mradi wana leseni inayomruhusu kununua madini.

Amefafanua kuwa mchakato wa mnada huo umefanyika kwa muda wa siku tatu na kesho Alhamisi Mei 14, 2026 ndiyo kutafanyika mauzo rasmi kwa wafanyabiashara watakaoshinda kupitia mtandao.

Katibu wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (Marema) Tawi la Mirerani, Rachel Njau amepongeza mchakato mzima wa mnada huo unavyofanyika kwa haki na bila ubaguzi wowote ule.

Njau amesema mnada huo umekaribisha wafanyabiashara wote wanunuzi wenye leseni wanajiandikisha na kununua madini kwa kutoa bei kupitia mtandao baada ya kuyakagua na kuridhia mwenyewe.

Mmoja kati ya wafanyabiashara walioshiriki mnada huo, Kalokola Mahamoud amesema mnada huo hauna ubaguzi.

“Kaseza amefanya mnada huu kwa kitaalamu mno, kwani amewaleta wafanyakazi wa taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha ya Tanzania Mercantile Exchange TMX kusimamia mnada,” amesema Kalokola.

Mfanyabiashara mwingine aliyeshiriki mnada huo, Khadija Ally amesema wanashukuru kwa kupata fursa ya kusajiliwa na kuwepo katika biashara hiyo kwa njia ya mtandao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *