Dar es Salaam. Viongozi wa sekta binafsi na maofisa mbalimbali wameitaka Serikali kuongeza kasi ya utekelezaji wa mageuzi ya uwekezaji, kuboresha mazingira ya biashara na kuharakisha miradi ya kimkakati ya miundombinu ili kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam jana Jumanne Mei 12, 2026 wakati wa mkutano wa majadiliano ya kila mwezi ulioandaliwa na Jukwaa la Watendaji Wakuu nchini (CEOrt) na kuwakutanisha viongozi wa Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kujadili fursa za uwekezaji na changamoto zinazoathiri uchumi wa Tanzania.
Mkutano huo uliofadhiliwa na Heritage Insurance, ulikuwa na kauli mbiu isemayo, kutoka sera hadi utekelezaji: Kufungua fursa za uwekezaji Tanzania.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Gilead Teri, alisema Tanzania imeendelea kujijengea nafasi kama kitovu cha uwekezaji kinachoshindana katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na maendeleo ya miundombinu, mageuzi ya sheria na uwekezaji katika rasilimali watu.
Teri alitaja sekta za nishati, sayansi na teknolojia, usafirishaji wa pamoja (integrated logistics), mageuzi ya kidijitali pamoja na utafiti na maendeleo kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha Dira 2050.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, akizungumza wakati wa mjadala ulioandaliwa na Jukwaa la Watendaj Wakuu Tanzania (CEO Roundtable of Tanzania -CEOrt) jijini Dar es Salaam.
Alisema mafanikio hayo yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Hakika kuna dhamira ya makusudi kwa sasa kuelekea kufanikisha malengo ya Dira 2050,” alisema Teri.
Alibainisha miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo uboreshaji wa reli, upanuzi wa bandari na maendeleo ya sekta ya usafirishaji inaonyesha namna Serikali inavyoendelea kuwekeza katika kuongeza ufanisi wa biashara na usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi.
“Ukizungumza na wadau wa usafirishaji, ongezeko la mizigo inayopita ni uthibitisho kuwa Tanzania inawekeza katika kasi na ufanisi,” alisema.
Aidha, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kupitia mageuzi ya kisera na kisheria yanayolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Alisema zilizochukuliwa katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo marekebisho ya sheria za uwekezaji na kuanzishwa kwa taasisi mpya za uwekezaji, zimechangia kujenga mazingira rafiki zaidi kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CEOrt, David Tarimo, alisema sekta binafsi ipo tayari kuunga mkono ajenda ya mageuzi ya kiuchumi ya muda mrefu, lakini akasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sera thabiti na mifumo madhubuti ya utekelezaji.
“Ufanisi wa Dira 2050 hautategemea tu sera nzuri bali pia uwezo wa kuweka mazingira wezeshi kwa biashara kuwekeza, kubuni na kupanuka,” alisema.
Alisema mazungumzo ya mara kwa mara kati ya sekta ya umma na binafsi ni muhimu katika kutafuta suluhisho la changamoto za kiuchumi na kuimarisha ushirikiano kuelekea maendeleo endelevu ya Taifa.
Mjadala huo umefanyika ikiwa ni wiki chache zimepita tangu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kuwasilisha bajeti yake ya mwaka 2026/27 akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza viwanda, kuongeza mauzo ya nje na kuimarisha uchumi wa muda mrefu chini ya Dira 2050.