Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imepanga kutoa uamuzi wa pingamizi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali usio sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar inayokikabili, Mei 20, 2026.

Uamuzi huo ndio utakaotoa hatima ya uhalali wa kesi hiyo,  kuendelea kuwepo mahakamani na hivyo kusikilizwa madai ya msingi au kutupiliwa mbali

‎Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

‎Wadaiwa katika kesi hiyo ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Awali wadaiwa waliibua pingamizi la awali wakiiomba mahakama hiyo iitupilie mbali pamoja na hoja nyingine wakidai kuwa imefunguliwa nje ya muda uliowekwa na Sheria ya Ukomo wa Muda, inayotaka kesi kama hiyo ifunguliwe ndani ya miaka sita tangu kutokea kwa sababu ya madai husika.

Hata hivyo Mahakama Kuu pamoja na kuamua hoja nyingine za pingamizi hilo, haikuitolea uamuzi hoja hiyo ya kufunguliwa nje ya muda, badala yake iliendelea na hatua nyingine za usikilizwaji wa kesi hiyo ya msingi pamoja na mashauri mengine madogo yaliyotokana nayo.

Baadaye Mahakama ya Rufani kwa maelekezo ya Jaji Mkuu, ilifanya mapitio ya kesi hiyo na mashauri madogo yaliyofuatia.

Katika uamuzi wake ilioutoa Aprili 15, 2026 Mahakama ya Rufani ilibatilisha sehemu ya mwenendo wa uamuzi wa Mahakama Kuu uliokizuia chama hicho kwa muda kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo itakapomalizika.

Pia mahakama hiyo ilielekeza kesi hiyo isikilizwe na jaji mwingine tofauti na jaji Hamidu Mwanga aliyekuwa akiisikiliza awali pia ikaelekeza jaji huyo mpya aanza kusikiliza pingamizi la Chadema kuhusiana na ukomo wa muda.

Pingamizi hilo limesikilizwa leo Mei 20, 2026 na Jaji David Ngunyale na baada ya kusikiliza hoja za pande zote akapanga kutoa uamuzi wake Mei 20, 2026.

Hoja za pingamizi

Kiongozi wa jopo la mawakili wa wadaiwa (watoa pingamizi) Mpale Mpoki ameieleza mahakama kuwa kesi haipaswi kuwepo mahakamani kwa kuwa waombaji hawakukidhi matakwa ya Amri ya VII kanuni ya 1(e) ya Kanuni za Mwenendo wa Mashauri ya Madai (CPC).

Amedai kuwa katika hati ya madai hakuna hata aya moja inayozungumzia kuwa ni lini sababu ya madai ilitokea na kwamba katika aya ya nne ya hati ya madai waombaji wanaeleza kuwa sababu za madai yao bila kueleza zilianza lini.

Wakili Mpoki kwa niaba ya mawakili wenzake, Dk Rugemeleza Nshala, Hekima Mwasipu na Selemani Matauka, amedai kuwa madhumuni ya matakwa ya kanuni ya 1(e) ni kuiwezesha mahakama kutambua kama kesi imefunguliwa ndani ya muda au la.

Huku akiirejesha mahakama katika uamuzi wa kesi mbalimbali zilizokwishakuamuliwa na Mahakama Kuu na zingine Mahakama ya Rufani, wakili Mpoki amedai kuwa kesi nyingine zimekuwa zikiondolewa mahakamani kwa kutokukidhi matakwa ya kanuni ya 1(e) ya CPC.

Amedai kuwa katika mashauri hayo Mahakama zimesema kuwa kama muda wa kuanza sababu za madai haujaonesha kunainyima mahakama uwezo wake wa kujua kama ina mamlaka ya kusikiliza kesi husika.

“Mheshimiwa kutokana na sababu tulizozisema ni rai yetu kwamba kesi hii haionyeshi muda wa kuanza madai na tunaiomba mahakama iitupilie mbali kwa gharama kwa sababu hizo,” amesema wakili Mpoki.

Majibu ya wadai

Akijibu hoja hiyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai (wajibu pingamizi), Shabaan Marijani amesema kuwa anakubaliana na hoja ya wadaiwa kwamba Amri ya VII kanuni ya 1(e) ya CPC inaeleza kuwa kesi lazima ieleze muda wa kuanza madai na kwamba kutokuonesha hilo ni kosa.

Hata hivyo amedai kuwa wanachotofautiana ni hoja kwamba katika kesi hiyo wadai hawajaonesha muda wa kuanza madai hayo.

Badala yake wakili Marijani amesema kuwa kesi hiyo imeonesha ni lini sababu za madai zilianza huku akiielekeza mahakama katika aya ya mbalimbali ya saba mpaka ya 16 ambazo nyingine zimetaja tarehe, mwezi na mwaka na nyingine zikionesha kuwa mambo wanayoyalalamikia yanaendelea mpaka sasa.

Wakili Marijani, akisaidiwa na mawakili Gido Simfukwe na Alvan Fidelis, amesisitiza kuwa kwa sababu hizo kesi hiyo imefunguliwa ndani ya muda wa ukomo kama inavyotakiwa kisheria.

“Hivyo basi haiwezi kuwa sahihi leo hii kuiaminisha mahakama hii kuwa kesi hii iko nje ya muda. Kwa hiyo shauri hili lililoko mbele yetu walalamikaji wameeleza msingi wa madai yao na muda ambao wao wanaamini yalitokea na walalamikiwa wamejibu bila kukanusha,” amesema wakili Marijani.

Katika hatua nyingine wakili Marijani amedai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 18(1) cha Sheria ya Ukomo wa Muda, imeondoa ukomo huo katika suala linalohusiana na mali.

Hivyo ameiomba mahakama ilitupilie mbali pingamizi hilo.

Hata hivyo kwa mara nyingine wakili Mpoki amesisitiza kuwa hili si suala la ushahidi na kwamba hilo bado ni pingamizi halisi la kisheria.

Kwa upande wake wakili Nshala amedai kuwa kifungu cha 18(1) cha Sheria ya Ukomo kinatumika tu pale panapokuwa na tuhuma dhidi ya wadhamini (kama watu binafsi) kutumia vibaya mali za taasisi na si dhidi ya bodi kama ilivyo katika kesi hiyo.

Wakili Nshala amesisitiza kuwa hakuna aya hata moja katika hati ya madai ambayo inazungumzia masuala ya mali bali mambo mengine kabisa na kwamba pia kuna mlalamikiwa wa pili ambaye ni Katibu Mkuu wa chama na si mdhamini, hivyo hawezi kufungwa na kifungu cha 18(1).

Kuhusu aya ambazo wajibu pingamizi wamedai kuwa ndizo zinazoonesha muda wa lini mgogoro ulianza akisema,  aya ya saba mpaka ya 14 haielezi ni lini mgogoro ulianza badala yake zinaeleza tu mambo wanayoyalalamikia.

Amesisitiza kuwa lazima kuwepo na maelezo yanayotaja tarehe ambayo mgogoro huo ulianza.

“Kwa mfano aya ya 20 haisemi kuwa tarehe fulani mahali fulani viongozi fulani walisema maneno ya kuvunja Muungano,” amesisitiza Dk Nshala na kuhitimisha;

“Kwa hiyo kutokana na kasoro kubwa zilizomo katika kesi hii mahakama yako inakuwa haina mamlaka ya kuisikiliza na ina kasoro zisizorekebishika na inatakiwa kufukuzwa.”

‎Katika kesi hiyo wadai wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na katiba ya chama hicho.

‎Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo pamoja na mambo mengine wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *