Dodoma. Spika wa Bunge, Mussa Zungu ameahirisha kwa muda shughuli za Bunge baada ya kubaini kuwa vipaza sauti ndani ya Ukumbi havifanyi kazi.

Mapema leo Alhamisi Mei 14, 2026 saa 2.59 asubuhi wakati Spika na timu ya makatibu walipokuwa wanaingia ukumbini wakiongozwa na mpambe wa Bunge, vipaza sauti (mix) vyote vilikuwa vimewaka lakini hakukuwa na sauti.

Hali hii imetokea ikiwa ni siku moja baada ya jana kusikika mlio wa king’ora ndani ya ukumbi ulioashiria kulikuwa na hali ya tafadhari na kufanya wabunge waondoke haraka ingawa baadaye Mwenyekiti wa Bunge, Deo Mwanyika alisema hakukuwa na tatizo na kikao kikaendelea.

Hitilifu ilianzia kwa kutosikika sauti ya mpambe anayebeba Siwa ambaye huonyesha ishara ya kiongozi kuingia ambaye alionekana akiachama mdomo lakini hakukuwa na sauti.

Baada ya kusimama kwenye kiti chake ili asome dua, sauti ya Spika haikuwa ikisikika na ghafla aliingia mpambe ambaye aliondoa Siwa sehemu yake na kuliweka kwenye droo ya meza ya mbele.

Spika aliondoka eneo lake na Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba naye alisimama kisha akaondoka.

Dakika chache baadaye waliingia wapambe wa Bunge wakalibeba Siwa katika sanduku maalumu na kutoka nayo nje wakati huo bado vipaza sauti vilionekana vikiwa vimewaka ukumbi mzima.

Taarifa zimeelezwa kuwa Bunge litaendelea baadaye katika Ukumbi wa Pius Msekwa ili kupisha marekebisho ndani ya ukumbi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *