Ikiwa ni wiki mbili zimepita tangu Tanzania iruhusiwe kuuza bidhaa zake katika soko la China bila ushuru, wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa ni fursa kubwa yenye manufaa kiuchumi hususani kwa wazalishaji wa ndani.

Uamuzi huo unatajwa kuwa unafungua mlango mpana kwa bidhaa za Tanzania kuingia katika moja ya masoko makubwa duniani kwa gharama nafuu zaidi, hali inayoweza kuongeza mauzo ya nje, uzalishaji wa viwandani na mapato ya fedha za kigeni.

Wataalamu wa uchumi wanasema upendeleo huo wa kibiashara unaweza kuwa na manufaa makubwa zaidi ikiwa bidhaa zitakazouzwa ni zile zitakazokuwa zimeongezewa thamani badala ya kupeleka malighafi.

Bidhaa kama kahawa, chai, korosho, pamba, viungo, bidhaa za baharini na madini zinapewa nafasi kubwa zaidi huku hatua hiyo ikitajwa kuwa moja ya njia inayoweza kusaidia kupunguza nakisi ya biashara, kuimarisha thamani ya shilingi kupitia ongezeko la fedha za kigeni na kuvutia uwekezaji.

Mei 10 mwaka huu, China ilitangaza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zitanufaika na mpango huo ulioanza rasmi Mei Mosi ukilenga kuboresha mahusiano ya kibiashara na ushirikiano wa kidiplomasia.

Akizungumzia suala hilo, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian alisema ushuru sifuri utafanya bidhaa za Tanzania kuwa na ushindani mkubwa zaidi katika soko la China ambalo lina watu zaidi ya bilioni 1.4.

 “Hii itasaidia kuongeza mauzo ya mazao ya Tanzania kama korosho, kahawa, ufuta, parachichi, mwani pamoja na madini kama Tanzanite na kinywe. Mazao ya Tanzania yana ubora mkubwa na sasa yatapata nafasi nzuri zaidi katika soko la China kutokana na kuondolewa kwa ushuru,” alisema.

Kwa hatua hiyo Tanzania inaungana na Kenya, Ghana, Nigeria, South Africa, Egypt, Ethiopia, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Morocco na Algeria zinazonufaika na mpango huu unaolenga kurahisisha bidhaa zao kuingia katika soko la China bila kutozwa ushuru ili kuongeza biashara na kukuza uchumi wa pande zote mbili.

Hili linafanyika wakati ambao ripoti ya mwaka ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayoishia Juni 2025 inaonyesha kuwa Tanzania iliuza bidhaa za Sh1.17 trilioni kwenda nchini China wakati ikiingiza bidhaa za Sh13.63 trilioni.

Akichambua fursa hiyo, Mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Profesa Samwel Wangwe amesema licha ya fursa hiyo kuwa adhimu lakini ni vyema kuhakikisha mazao hayo kabla ya kuuzwa yanaongezewa thamani.

“Yaongezewe thamani hapa na ikiwezekana kama teknolojia inakuwa shida kampuni ya kutoka China iingie ubia na Tanzania ili tuongeze thamani huku kabla ya kupeleka nje ya nchi,” anasema.

Anasema kinyume na hapo, kuendelea kuuza malighafi hakutainufaisha sana nchi ukilinganisha na kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani jambo ambalo linapaswa kuongezwa.

Ili kuhakikisha wafanyabiashara wanafikia soko hilo kikamilifu, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha wafanyabiashara wanaelewa taratibu za kuuza bidhaa China.

 “Mpango huu si wa kuondoa kodi tu, bali ni wa kuleta ustawi kwa wakulima, wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania,” alisema na kuongeza kuwa serikali haitawaacha wafanyabiashara peke yao katika safari hii mpya ya kibiashara, bali itaandamana nao hatua kwa hatua.

Kufanikisha hilo kutakuwa na mfumo maalum wa uratibu wa mauzo ya nje, ambapo mfanyabiashara ataanzia pale anapoandaa bidhaa, hadi inafika sokoni China, bila kukwama njiani.

 “Hatutaki mfanyabiashara abaki katikati akishindwa kujua aende kwa nani au afuate hatua gani, tutakuwa na mfumo mmoja wa kumsaidia kuanzia mwanzo hadi mwisho,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kapinga alisema Serikali imeanza kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuhakikisha huduma zote za biashara zinafuatiliwa kwa uwazi.

 “Hii itawawezesha wafanyabiashara kufahamu hatua ya maombi yao bila kuchelewa au kupoteza muda katika ofisi mbalimbali,” amesema.

Alizitaka taasisi zote za udhibiti kubadilika na kuwa taasisi za kuwezesha biashara badala ya kumzuia mfanyabiashara kwa sababu hajafikia kiwango fulani, 

“Taasisi hizo zitaelekezwa kumsaidia kufikia viwango vinavyohitajika ili aweze kushiriki kikamilifu kwenye soko la kimataifa,”

“Pia, kwa kushirikiana na Ubalozi wa China na wadau wa biashara, serikali itawawezesha wafanyabiashara kupata taarifa sahihi za soko, mafunzo ya lugha na uelewa wa taratibu za biashara za kimataifa ili kupunguza changamoto zinazoweza kuwazuia kufanikiwa,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara alisema Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuwasaidia wafanyabiashara kutumia kikamilifu fursa hiyo.

Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za biashara za kimataifa pamoja na kuhakikisha bidhaa zinakidhi viwango vya ubora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *