Baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu, mradi wa Mchuchuma na Liganga sasa unaingia katika hatua ya utekelezaji, ukiibua matumaini mapya kwa uchumi wa Tanzania.

Miradi huo ambao kwa miaka mingi umekuwa ukitajwa kama mkombozi wa sekta ya viwanda, ajira na nishati, umepitia danadana nyingi za mikataba, uwekezaji na maandalizi ya miundombinu kabla ya kufikia hatua hii inayosubiriwa kwa hamu.

Kwa kuanza rasmi kwa utekelezaji wake ndani ya miezi mitatu ijayo kama ilivyosemwa na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, wachambuzi wanaona Tanzania inakwenda kunufaika kwa njia nyingi ikiwamo uzalishaji wa chuma cha ndani, kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa za chuma kutoka nje.

Pia mradi huo unatazamiwa kufungua fursa za ajira kwa wananchi, kuchochea maendeleo ya mikoa ya Kusini, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha safari ya taifa kuelekea uchumi wa viwanda.

Haya yanawekwa bayana ikiwa ni siku chache tangu Msigwa awaambie waandishi wa habari kuwa mradi wa makaa ya mawe na chuma wa Liganga na Mchuchuma unaotekelezwa wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe, unatarajia kuanza miezi mitatu ijayo.

Msigwa anasema Serikali imeamua kutatua changamoto na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Mkoa wa Njombe kutokana na kuchelewa kuanza kwa mradi huo na sasa Serikali ipo zaidi ya asilimia 90 kukamilisha mazungumzo na baada ya miezi mitatu ijayo.

Ndani ya kipindi hicho, wananchi wataanza kuona matokeo ya uwekezaji mkubwa katika mradi huo wa kimkakati na kielelezo, ambao unategemewa kuzalisha ajira zaidi ya 6,500 na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 26,000 na kuiwezesha Tanzania kupata bidhaa ya chuma ya kutosha.

Ndani ya mradi huo utakuwepo uzalishaji wa mradi wa umeme wa Megawati 600 na kwa sasa mwekezaji anakamilisha taratibu za mwisho ili mradi huo uanze.

“Pia mradi utakuwa na uwezo wa kuzalisha chuma ghafi 2.9 trilioni kwa mwaka huku bidhaa za chuma zikizalisha tani 1.1 milioni kwa mwaka. Mgodi wa makaa ya mawe utazalisha tani milioni 3 za makaa ya mawe,” anasema.

Anasema watafiti wamebaini kuwa makaa ya mawe yaliyopo nchini ni zaidi ya tani bilioni 5 na Tanzania ni moja ya nchi yenye makaa mengi ya mawe na bora na yataanza kuzalishwa katika mradi huo wa Liganga na Mchuchuma.

Anasema miaka ishirini na tano ya kwanza ya mradi huo wanategemea Serikali itapata mapato ya Dola 1.9 bilioni za Marekani ni sawa na zaidi ya Sh5.17 trilioni kutokana na uwekezaji wa mradi huo.

Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika mwaka 2013 kuhusu uwepo wa madini hayo ziligundua uwepo wa tani milioni 428 za makaa ya mawe katika eneo la ukubwa wa mraba 30 ambazo zinaweza kuchimbwa kwa miaka zaidi ya 140 na Chuma ambacho ni zaidi ya tani milioni 126 kinachoweza kuchimbwa kwa miaka 58.

Mei 9, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaagiza Wizara ya Viwanda na Biashara na ile ya Mipango na Uwekezaji kukamilisha mchakato wa kuipata kampuni itakayowezesha kuanza kwa mradi huo akilenga kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya kiwanda cha kuzalisha magari makubwa cha Saturn Corporation Limited kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda hicho Samia alisema zipo malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa magari ikiwamo vioo na vyuma.

“Hivyo nikuombe Waziri wa Viwanda na Mwenzako wa Uwekezaji, malizieni suala la Liganga na Mchuchuma, tupate kampuni bora itakayoanza kuchimba chuma ile ili iwe malighafi katika viwanda hivi, niwaombe saa hili limaliziwe kwa haraka ili tuweze kupata,” aliagiza.

Wasemavyo wachambuzi

Mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Dk Yohana Lawi anasema japokuwa ni jambo linalopaswa kupongezwa kufuatia kuanza rasmi kwa mradi huo lakini ni wazi kuwa umechelewa.

Anasema licha ya umuhimu wa makaa ya mawe kama chanzo kikuu cha nishati lakini umuhimu wake unapungua zaidi duniani tofauti na miaka ya nyuma kwani inachangia uharibifu wa mazingira kutokana na kuzalisha kwa hewa ukaa.

“Nchi nyingi zinapunguza matumizi yake na kumekuwapo na mikataba mbalimbali ambayo imekuwa ikisainiwa kupunguza matumizi ya makaa ya mawe,” anasema.

Kwa sababu Tanzania imefikia hatua hii wakati ambao bado kuna matumizi ya makaa ya mawe katika nchi chache duniani ni vyema kwenda na kasi hiyo kuhakikisha uzalishaji unafanyika kwa wingi na yanatumika ipasavyo ili kufikia malengo yaliyowekwa.

“Lakini sehemu tunayozalisha makaa ya mawe pia kuna chuma. Makaa ya mawe yatumike kama nishati kwa ajili ya kutengeneza chuma, tusiuze chuma kama malighafi nje ya nchi, tuhakikishe makaa ya mawe yaliyopo yatumike katika kuongeza thamani,” anasema.

Kufanya hivyo Tanzania itakuwa miongoni mwa wazalishaji wa chuma Afrika, itauza na kuleta ongezeko la mapato ya kikodi, kuongeza ajira kwa vijana waliohitimu katika vyuo vya kati na elimu ya juu na wananchi wanaozunguka eneo hilo.

“Pia ni njia ya kuweza kujenga viwanda vingine vitakavyokuwa vinahusiana na chuma. Twende mbali zaidi tutengeneze na viwanda vinavyotegemea chuma, viwanda vya magari tufikie hatua hiyo kwani sasa tuna uwekezaji na ushirikiano wa nchi na viwanda vingine kwani sasa kuna uhakika wa nishati na chuma,” anasema.

Anasema ni wakati wa kuangalia namna ya kuvuta wawekezaji wanaoweza kutumia chuma katika kufanya uwekezaji ili kuboresha mnyororo wa kiuchumi na kuukamilisha.

Anasema kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaonyesha kuwapo kwa ujenzi wa treni ya umeme (SGR) kati ya Mtwara hadi Mbambabay hivyo matarajio yake ni kuona chuma kitakachotumika katika ujenzi huo basi kitoke Liganga.

“Kufanya hivi kunatoa uhakika wa viwanda vipya kwa sababu kutakuwa na njia ya usafirishaji wa uhakika wa bidhaa kutoka katika eneo la viwanda. Eneo hili linaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi hasa kwa kuongeza thamani ya chuma kitakachochimbwa pale,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Sera za Umma (Repoa), Dk Donald Mmari anasema mradi huo utaleta mageuzi katika uchumi wa Tanzania kwani ujenzi wa viwanda vikubwa unapofanyika hutegemea maligafi ya chuma.

“Kwa sasa tunaingiza sana malighafi ya chuma kutoka nje na huu msukosuko duniani uliotokea umefanya gharama za uchukuzi, bei vyote vimepanda sana, hayo yakifanyika huko huku pia bei inaongezeka,” anasema.

Kuanza kwa mradi nchini inaleta ahueni kubwa hasa katika sekta ya ujenzi na miundombinu kama reli ambazo zinajengwa kwa kutumia chuma.

“Hii inaweza kufanya uzalishaji wetu ukawa wa ushindani, gharama nafuu, ikaongeza ajira kwani sekta hiyo inachukua watu wengi na mnyororo wa thamani itaongezeka,” anasema.

Nchi kinara uzalishaji chuma

Kwa mujibu wa Shirikisho la wazalishaji chuma duniani, China ndiyo nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa chuma ghafi duniani ambapo kati ya Januari hadi Desemba mwaka jana ilizalisha tani milioni 980.

India ilikuwa nafasi ya pili ikiwa na tani milioni 164.9, Marekani tani 82 milioni, Japan tani 80.7 milioni, Urusi ikiwa na tani 67.8 milioni, Korea kusini ikiwa na tani 61.9 milioni, Uturuki ikiwa na tani 38.1 milioni huku Ujerumani ikizalisha tani  34.1 milioni.

Nchi ya Brazil ikiwa nafasi ya tisa duniani kwa kuzalisha tani 33.3 milioni na Iran ikifunga kumi bora kwa kuwa na uzalishaji wa tani 31.8 milioni.

Kwa upande wa Afrika nchi zinazoongoza katika uzalishaji kwa mujibu wa tovuti hiyo ni Algeria, Misri, Libya, Morocco, Afrika Kusini na Tunisia hivyo kuanza kwa mradi huo kutaiweka Tanzania nayo katika ramani ya wazalishaji wa bidhaa hiyo muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *