
Watu zaidi ya 80 wamefariki dunia baada ya dhoruba kali iliyoambatana na mvua kubwa ya mawe kulikumba Jimbo la Uttar Pradesh nchini India, ambalo ndilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu nchini humo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Reuters, Ofisi ya Usimamizi wa Maafa na Misaada ya jimbo hilo imesema hali mbaya ya hewa iliyotokea Jumatano ilisababisha vifo vya watu 89.
Dhoruba hizo ambazo hutokea mara kwa mara katika maeneo ya kaskazini mwa India wakati wa msimu wa joto kati ya Machi na Juni, kabla ya kuanza kwa mvua za masika, zilisababisha pia majeruhi 53, uharibifu wa nyumba 87 pamoja na vifo vya mifugo 114.
Kamishna wa misaada Uttar Pradesh amesema kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wa X kuwa mvua kubwa, upepo mkali, radi pamoja na mvua ya mawe vilisababisha madhara katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Picha zilizoonyeshwa na vituo vya televisheni nchini India zilionyesha miti na mabango makubwa yakiong’olewa na upepo mkali huku baadhi yake yakidondokea magari katikati ya vumbi na vifusi vilivyosambaa barabarani.
Pia, samani za vibanda vya biashara zilizokuwa kandokando ya barabara zilionekana kutawanywa na nguvu ya upepo.
Baadhi ya vifo vilielezwa kusababishwa na miti kuanguka pamoja na kuta za nyumba kuporomoka kutokana na nguvu ya dhoruba hizo.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amewaagiza maofisa kuwasaidia waathirika na kuhakikisha misaada ya kifedha inatolewa ndani ya saa 24.