Dar/Mikoani. Kuna mechi nne za Ligi Kuu Tanzania Bara zinachezwa leo Alhamisi huku vita ya pointi tatu ikitarajiwa kusakwa kibabe kuanzia saa nane mchana. Katika vita hiyo, kuna zinazohitaji kuweka heshima, zingine zikipambana kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo.
Mapema saa 8:00 mchana, Mtibwa Sugar itaikaribisha KMC, kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Mtibwa inarejea kucheza nyumbani kwenye Uwanja wa Jamhuri baada ya kifungo cha muda mrefu huku ikisaka pointi za kujiimarisha kwenye msimamo.
Katika mechi tano zilizopita, Mtibwa haijashinda mchezo wowote ikipoteza minne na kutoa sare moja. Mara ya mwisho kushinda ilikuwa Februari 2, 2026 ilipoifunga Prisons mabao 2-1. Walima miwa hao wanahitaji ushindi ili kupanda kutoka nafasi ya 12 hadi ya 10 kwenye msimamo.
Hali hiyo haipo tofauti kwa KMC ambayo nayo ipo kwenye hatari ya kushuka daraja. Mara ya mwisho kushinda ilikuwa Februari 3, 2026 ilipoifunga Mashujaa bao 1-0. Iwapo KMC itapoteza mchezo wa leo, itaendelea kubaki karibu zaidi na eneo la kushuka daraja ikiwa nafasi ya 16 na pointi tisa.
Beki wa Fountain Gate wakati akijaribu kumzuia mshambuliaji wa Pamba Jiji katika mechi ya Ligi Kuu Bara. Picha na Pamba Jiji
Kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Tanzania Prisons itakuwa mwenyeji wa Fountain Gate ambapo mechi hiyo nayo itaanza saa 8:00 mchana.
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa katika kuelezea maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Fountain Gate, alisema watashambulia mwanzo mwisho, huku akiwa na kumbukumbu kwamba hajashinda mechi yoyote kikosini hapo kati ya tisa, presha imeonekana kuwa kubwa nje na ndani ya uwanja katika hesabu za kukwepa kushuka daraja.
Prisons haijawa na matokeo mazuri ikiwa nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 14, ambapo leo Nsajigwa atakuwa akisaka ushindi wa kwanza kwake tangu aungane na Wajelajela hao dhidi ya Fountain Gate ambayo imeonekana kuimarika chini ya Kocha Fred Felix ‘Minziro’.
Katika michezo 22 iliyocheza timu hiyo ya jijini Mbeya, imekusanya pointi 14 na kuwa nafasi ya 15 ambapo inahitaji ushindi mechi zilizobaki kujihakikishia kubaki salama Ligi Kuu Bara.
“Tumeshafungwa sana, ila sisi hatujashinda, kesho (leo) ni kushambulia tu kusaka mabao na kulinda pointi tatu, vijana nimewaandaa kiakili, kimbinu na kiufundi ili tuianze upya safari ya matumaini.
“Tunajua rekodi na historia yetu nyuma kwamba kila msimu huwa tuna mechi zinazotubeba hadi kubaki, hivyo hatujakata tamaa na tunaweza kubaki salama, ila lazima tushinde michezo hiyo,” alisema Nsajigwa.
Naye Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Fred Felix ‘Minziro’ alisema: “Wachezaji wako tayari kwa mchezo na sisi hatuko salama sana, tunaenda kwa nidhamu, heshima na tahadhari katika mchezo huo kwa kuwa Prisons ni timu nzuri, ukifanya makosa wanakuadhibu.”
Kiungo wa Simba, Clatous Chama wakati akithibiti mpira katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons iliyopigwa Mei 10, 2026. Picha na Simba
Saa 10:15 jioni, Simba itakuwa mgeni wa Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa kwenye ubora mkubwa wa matokeo ambapo mechi tano zilizopita imeshinda nne na kutoka sare moja dhidi ya Yanga. Katika michezo hiyo, Wekundu hao wamefunga mabao 13 na kuruhusu matatu pekee huku wakiendelea kuifukuzia Yanga iliyo kileleni mwa msimamo.
Hata hivyo, Mashujaa inayonolewa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ina rekodi ya kutopoteza nyumbani msimu huu ikishinda nne na sare saba.
Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Simba, Steve Barker, alisema: “Nilikuwa naangalia mechi ya mwisho tulipocheza nao, ilikuwa ngumu, naamini pia haitakuwa rahisi safari hii kwani ni timu inayoonyesha upinzani mkubwa ikiwa nyumbani, lakini tunataka kuendelea kushinda, naamini wachezaji wangu watatekeleza vizuri mpango wa mechi hii.”
Kocha Julio alisema licha ya kuheshimu ubora wa Simba, lakini kikosi chake hakitakuwa na hofu mbele ya Wekundu hao.
“Tunaiheshimu Simba lakini kama ambavyo siku zote nimekuwa nikisema, sidhani kama tuna sababu ya kucheza kwa hofu dhidi yao, nimewaambia wachezaji hizi ndio mechi ambazo zitawatambulisha juu ya ubora wao, tutakwenda kuwapa shida kucheza kwa utulivu wao,” alisema Julio ambaye tangu aichukue Mashujaa, timu hiyo haijapoteza mchezo wowote.
Saa 12:30 jioni, Azam baada ya kutoka kuchapwa mabao 4-1 na TRA United, itakuwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuikaribisha Pamba Jiji.
Nahodha wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda wakati akijaribu kuzuia moja ya shambulizi dhidi ya TRA United katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Ijumaa Mei 8, 2026. Picha na Azam FC
Kipigo ilichopokea kutoka kwa TRA United, kilikuwa cha kwanza kwa Azam kwenye ligi msimu huu, hivyo itaingia kwa hasira kulinda rekodi ya kutopoteza nyumbani kwani imeshinda sita na sare nne.
Azam imesisitiza kuwa inataka kurejea kwenye njia ya ushindi huku ikikumbuka kwamba mchezo wa kwanza dhidi ya Pamba Jiji uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 ulikuwa mgumu kwao.
Kwa Pamba Jiji, haina rekodi nzuri ikiwa ugenini kwani imeshinda mechi mbili pekee, huku ikipoteza tano na sare nne. Mechi nane zilizopita, Pamba Jiji imeshinda moja pekee, sare zikiwa nne na vichapo vitatu.