Musoma. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amepiga marufuku michango iliyokuwa ikitozwa na baadhi ya shule za sekondari katika Manispaa ya Musoma kwa maelezo kuwa michango hiyo inakichonganisha chama hicho na wananchi.

Kihongosi ametoa agizo hilo kufuatia malalamiko yaliyotolewa na mkazi wa Musoma, Lucia Etwana aliyeomba msaada wa Sh600,000 kwaajili ya kulipia masomo ya mwanaye anayesoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya kutwa Makoko katika manispaa hiyo.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara mjini Musoma leo Mei 14, 2026 Kihongosi amesema michango hiyo inaleta ukakasi kutokana na kuwa ni kiwango kikubwa huku tayari Serikali ikiwa imeelekeza nini cha kufanya endapo kutakuwa na ulazima wa wazazi kuchanga fedha kwaajili ya elimu kwa shule za msingi na sekondari.

Amesema Serikali tayari imetangaza elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita na kwamba  michango inayoruhusiwa kutolewa ni ile  ambayo inatokana na makubaliano kati ya wazazi na shule kupitia uratibu maalum wa uongozi wa halmashauri na ofisi ya mkuu wa wilaya.

“Mchango wa Sh600,000 kwa mwananchi wa kawaida hii sio sawa kabisa, mnaleta uchonganishi kati ya chama na wananchi hili sitalikubali, nakuagiza mkurugenzi kaa na watu wako pitia shule zako zote uone utaratibu ukoje, mnakiuka maelekezo ya Serikali nawaheshimu sana watumishi wa umma lakini kwenye hili hapana,” amesema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amepiga marufuku michango iliyokuwa ikitozwa na baadhi ya shule za sekondari katika Manispaa ya Musoma kwa maelezo kuwa michango hiyo inakichonganisha chama hicho na wananchi.

Amesema siyo lazima mzazi kutoa fedha pale ambapo panahotajika michango mfano mzazi anaweza kuchangia mahindi au maharage badala ya kulazimisha wazazi kutoa fedha taslimu.

Awali, Lucia Etwana aliomba kupewa fedha kwaajili ya kulipia kambi ya mafunzo kwaajili ya mwanae ambaye yupo kidato cha nne shuleni hapo kwa maelezo kuwa hana uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha.

“Watoto wote wa kidato cha nne wanatakiwa kwenda kambini kwaajili ya kujiandaa na mitihani yao sasa mimi sina uwezo huo naomba nisaidiwe,” amesema.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma,  Bosco Ndunguru amesema shule hiyo ya Makoko ni ya kutwa na kwamba wanafunzi wanaokaa hosteli wanafanya hivyo kwa hiari.

“Naomba hili suala nilifanyie kazi ila suala la malipo pale shuleni tunalifahamu ni hayo malipo ni kwaajili ya chakula na huduma zingine kwenye ile hosteli kama vile maji na umeme,” amesema Ndunguru.

Kihongosi pia amewataka watumishi wa umma kutenda haki bila upendeleo huku akisema wapo baadhi ya watumishi wa umma ambao wamegeuka kuwa miungu watu huku wakiendelea kuwanyanyasa watu hasa wenye kipato duni.

Agizo hilo amelitoa baada ya mkazi wa Manispaa ya Musoma, Nuru Wandwi kudai kunyang’anywa eneo lake aliloandaa kwaajili ya biashara ya kuosha magari na kupewa mtu mwingine ambaye hakutaja jina lake.

“Nimezuiliwa kufanya biashara yangu pale Nyasho lakini cha kushangaza eneo amepewa mtu mwingine na anafanya bishara kama hiyo hiyo ya kwangu ya kuosha magari naomba mnisaidie,” amesema.

Kutokana na malalamiko hayo, Kihongosi amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma kumpa taarifa kamili juu  ya kwanini mmiliki wa eneo hilo amezuiliwa kufanya biashara katika eneo lake na kupewa mtu mwingine.

“Kesho saa tatu nataka nipate jina la huyo mtu aliyepewa eneo hilo nataka nijue ni nani na mbaya zaidi naambiwa hata uongozi wa mkoa ulikwishaagiza mwenye eneo apewe eneo lake lakini mmekaidi,” amesema.

Amesema watumishi wa umma wanapaswa kutambua kuwa kila mtu ana haki ya kupata huduma sawa bila kujali uwezo wake kifedha huku akiwatka kuwa na hofu ya Mungu kwani vyeo na madaraka ni vitu vya kupita, hivyo hakuna sababu ya kuleta maumivu kwa watu wengine kwa kutumia vyeo na nafasi zao.

Amesema chama hicho hakipo tayari kuona watumishi wachache wakitumika kuwaumiza wananchi wa hali ya chini kwa maslahi yao binafai na watu wao wanaowapendelea.

Mbunge wa Musoma Mjini, Mgore Miraji amesema Serikali ya CCM inaendelea kutayua changamoto za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa jimbo hilo.

Amesema kwa kuanzia tayari Serikali imetoa zaidi ya Sh19.9 bilioni kwaajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa na soko la kisasa pamoja na barabara za ndani mjini hapo miradi hiyo ikikamilika itachochea uchumi wa wakazi wa jimbo hilo.

“Kuhusu viwanda tayari mwekezaji wa kiwanda cha nguo cha Mutex amepatika na atawekeza zaidi ya Sh120 bilioni, muda si mrefu mikataba itasainiea na kazi ya kufufua kile kiwanda itaanza,” amesema Mgore.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *