Kigogo Super Falcon kuja kivingineKigogo Super Falcon kuja kivingine

ALIYEKUWA Mdhamini Mkuu na Rais wa timu ya Super Falcon, Hafidh Nassor ‘Hafidh Julian’ ameliambia Mwanaspoti kuwa, bado ana mpango wa kurudi kuwekeza kwenye Ligi Kuu Zanzibar.

Kigogo amesema kwasasa anajipanga kutafuta njia na mbinu za kisasa zitakazoendana na mabadiliko ya soka ili kurudi kuwekeza tena.

“Nina mpango mzuri wa kurudi kuwekeza kwenye ligi, ila nitarudi kivingine sio kwa utaratibu wa zamani,” amesema.

Amesema aliacha kila kitu kwenye soka wakati huo kwa sababu alichukizwa kuona baadhi ya watu wanafanya jitihada za makusudi kuishusha Super Falcon iliyokuwa na malengo ya kutetea ubingwa wake msimu wa 2012-2013.

Baada ya timu hiyo kupotea Ligi Kuu na sasa ikiwa inafanya vibaya Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Pemba, wengi hawakutambua alipoenda mdhamini huyo.

Hivyo, amesema yupo na wadau wa soka Zanzibar watulie kwani anajipanga kurudi kuendelea alipoishia.

Jina la mdhamini huyo sio geni baada ya kuweka historia nzuri kwa timu ya Super Falcon yenye makao makuu Kijiji cha Chanjanjamwiri, Wilaya ya ChakeChake kisiwani Pemba kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2011-2012.

Wakati timu hiyo inachukua ubingwa mbali na kuwa mdhamini, pia alikuwa Rais wa Super Falcon na kuifanikisha kuweka historia ikiwemo kuwa timu ya kwanza kwa wilaya ya hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *