Azam TV yaweka rekodi, kuonyesha mechi zote 104 Kombe la DuniaAzam TV yaweka rekodi, kuonyesha mechi zote 104 Kombe la Dunia

Kwa mara ya kwanza katika historia, kituo cha luninga cha Azam TV kitaonesha mbashara mechi zote 104 za Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Canada, Marekani na Mexico kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.

Hii inakuwa mara ya kwanza kwa televisheni ya Tanzania kuonesha mubashara mechi zote za Fainali za Kombe la Dunia tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo makubwa ya dunia mwaka 1930.

Pia, ni mara ya kwanza kwa Azam TV kupata haki ya kuonesha mechi zote za Kombe la Dunia tangu kampuni hiyo ilipoanzishwa mwaka 2013.

Azam TV itaonesha mechi hizo kupitia chaneli za Azam Sports 2HD na Azam Sports 4HD kuanzia mechi ya kwanza kati ya Afrika Kusini na Mexico Juni 11 na kumaliza kwa mchezo wa fainali utakaopigwa Julai 19, mwaka huu.

Wakati wa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, mechi ya kwanza ilikuwa kati ya Afrika Kusini na Mexico kama itakavyokuwa mwaka huu.

Utamu ni kwamba mechi zote zitatangazwa na kuchambuliwa kwa lugha adhimu ya Kiswahili zikiwa na ladha maalumu kutoka kwa watangazaji na wachambuzi mahiri wa soka nchini.

Kwa watazamaji wa nje ya Tanzania kama Malawi, Kenya na Uganda watapata uhondo huo kwa lugha ya Kiingereza kutoka kwa watangazaji na wachambuzi kutoka nchi husika.

Takribani nchi zote ambako Azam TV hufikisha matangazo yake watafaidi uhondo huo wa mechi.

Azam TV itakuwa na studio mbili za kisasa kwa ajili ya wachambuzi wa lugha ya Kiswahili na nyingine kwa Kiingereza.

Azam TV imezindua  kampeni yake kubwa ya matangazo hayo leo Jumamosi kwa kutumia helikopta maalumu inayozunguka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ikiwa na bango lenye maandishi ya: “Mechi zote 104,.

Argentina wanaingia katika fainali za mwaka huu wakiwa mabingwa watetezi wa taji hilo walilolitwaa mwaka 2022 baada ya kuifunga Ufaransa katika mechi ya fainali kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya dakika 120 za mechi hiyo kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Kwa mara ya kwanza katika historia, bara la Afrika litawakilishwa na timu 10 katika fainali hizo ambazo pia kwa mara ya kwanza zinaandaliwa na nchi tatu.

Wawakilishi 10 wa Afrika katika fainali hizo ni Senegal, Morocco, Tunisia, Afrika Kusini, Cape Verde, Misri, Algeria, Ghana, DR Congo na Ivory Coast.

Azam ndiyo kituo kikubwa cha televisheni nchini Tanzania ambacho kimekuwa kikifuatiliwa na watu wengi zaidi ukanda huu, kikiwa kinaonyesha pia Ligi Kuu ya NBC, michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho Afrika, Ligi ya Saudi Arabia, Ligi Kuu ya Kenya, La Liga, Bundesliga na nyingine nyingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *