
Simiyu. Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) imetumia mbinu ya kuwafunga mikanda yenye visukuma mawimbi (GPS) tembo viongozi ili kudhibiti uvamizi wa wanyama hao katika vijiji zaidi ya 12 wilayani Meatu.
Wananchi katika maeneo yenye migongano na tembo wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kama mabomu baridi na njia nyingine nyingi kukabiliana na kadhia hiyo.
Kwa mujibu wa Mtafiti na daktari wa wanyamapori kutoka Tawiri, Dk Iddi Lipende mikanda iliyofungwa itakuwa ikitoa taarifa za mienendo ya tembo watakapokuwa wanaelekea kwenye makazi na mashamba ya wananchi.
Akizungumza Mei 15, 2026 wilayani Meatu, Dk Lipende amesema askari wanyamapori waliopo kwenye vituo vya udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu, watapata taarifa mapema na kuwazuia kabla hawajasababisha madhara kwa wananchi.
Amesema mbinu hiyo ya GPS ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Maliasili na Utalii za kupunguza migongano kati ya wanyama na wananchi.
Ofisa Wanyamapori wa Wilaya ya Meatu, Joseph Sikawa amesema wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya uvamizi wa tembo mashambani, ambapo makundi ya tembo yamekuwa yakiingia katika vijiji vya Mwanyahina, Mwajidalala, Mwanzagamba, Mbugayabanya, Mwamashimba, Mang’wina, Mwangudo, Mbushi, Shushumi, Mbuyuni, Sungu na Paji.
Mkazi wa Meatu, Godfrey Mabula, amesema anafurahishwa na hatua hiyo kwa kuwa awali walilazimika kulala mashambani kulinda mazao yao dhidi ya tembo.
“Sasa teknolojia hii itasaidia kuwafuatilia wanyama hao mapema na kuwazuia kabla hawajafika katika maeneo yetu ya kilimo,” amesema Mabula.
Ofisa Uhifadhi Daraja la Kwanza kutoka Tawa, Ayubu Fundi, amesema wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuwarudisha tembo hifadhini, lakini wakati mwingine wamekuwa wakichelewa kuwafikia kutokana na wanyama hao kutoka maeneo mbalimbali ya hifadhi.
“Matumizi ya vifaa hivyo yatawezesha udhibiti wa haraka zaidi kabla ya tembo hao kuingia kwenye mashamba ya wananchi,” amesema Fundi.
