
Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema licha ya Serikali kujenga miundombinu mikubwa ya elimu, bado kuna kazi ya kuhakikisha inaendana na ubora wa elimu.
Wametolea kauli hiyo leo, Mei 16, 2026 wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA) katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Unguja, Zanzibar.
Wizara hiyo imeidhinishiwa na baraza Sh1.1 trilioni katika kutekeleza vipaumbele vyake sita mwaka 2026/27.
Akichangia bajeti hiyo, Mwakilishi wa Amani, Masoud Amour Masoud (CCM), amesema licha ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika majengo ya ghorofa ya shule za msingi na sekondari, bado watu wengi, wakiwemo wawakilishi wenyewe, hawapeleki watoto wao katika shule hizo.
“Lazima tuwe wakweli hapa, tunasifu majengo mazuri lakini hata sisi wenyewe humu wengi wetu hatupeleki watoto kwenye shule hizo, sababu kubwa ni moja, bado hakuna ufundishaji wa Kiingereza,” amesema.
Ameshauri wizara iangalie namna ambavyo itaboresha zaidi mitalaa. “Kiingereza kimekuwa shida, mtoto akianza darasa la kwanza mpaka la saba, masomo yote ni Kiswahili isipokuwa somo la Kiingereza. Akienda sekondari, masomo yote yanakuwa kwa Kiingereza isipokuwa Kiswahili tu.”
“Sasa ukiangalia mfumo huu hauwezi kutuletea mabadiliko ya elimu. Kwa hiyo ikiwezekana, mtoto asome mpaka darasa la nne masomo kwa Kiswahili, kisha kuanzia hapo mpaka la saba masomo yawe kwa Kiingereza,” amesema.
Amesema bado elimu ya Zanzibar ni ya kukaririsha mtoto na si kumfanya aelewe jambo, linaloshusha kiwango cha elimu.
Naye Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayub (CCM), amesema kuna mchanganyiko wa Kiarabu katika baadhi ya vitabu vya elimu Zanzibar, jambo ambalo amesema ni kosa kuchanganya elimu na dini.
“Ubora wa elimu, vitabu tunachanganya Kiarabu na dini, hapa haya ni makosa makubwa. Dini inatakiwa ibaki ijitegemee na vitabu vya elimu visichanganywe,” amesema.
Mwakilishi wa Chaani (CCM), Juma Usongi, amesema ipo haja ya kuanza kufundisha historia kuanzia ngazi za chini ili kuwajengea msingi mzuri, kwani Taifa ambalo halina historia haliwezi kufika popote.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtambwe kupitia ACT Wazalendo, Dk Mohamed Ali Suleiman, amesema Serikali bado haijaweka mkazo wa kutosha katika elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, kwani licha ya kujengwa kwa miundombinu ya shule, kundi hilo bado linakabiliwa na vitendo vya ubaguzi na kutengwa.
“Tunaambiwa watu wenye mahitaji maalumu kwenye hizi shule za ghorofa wao wakae madarasa ya chini; hii ni kuendeleza kuwanyanyapaa, kwani wao hawataki kukaa kwenye maghorofa. Tunatakiwa kuweka miundombinu kwa ajili yao,” amesema Dk. Mohamed.
Mwakilishi kwa nafasi za Wanawake, Tabia Maulid Mwita, amesema kuna baadhi ya maeneo walimu wanaofundisha hawana sifa na hawajasomea taaluma hiyo, hivyo kuitaka Wizara kuhakikisha walimu wanaofundisha wanafunzi hao wathibitishwe na wawe na taaluma husika.
Mwakilishi wa Chambani, Mahmoud Shineni Ali, amesema elimu ya msingi na maandalizi ndio msingi wa elimu, lakini bado hakujawa na mkazo mkubwa katika eneo hilo.
Amesema wanapaswa wasichukue kujua kusoma na kuandika kama ndio kiashiria cha elimu, badala yake wajikite katika ubora zaidi.
Pia, amesema wahitimu wa elimu mbadala hawana uwezo wa kiushindani kwani bado wanafundishwa nadharia zaidi badala ya vitendo.
“Tunapoteza fedha nyingi kujenga majengo makubwa ya maktaba, wakati tukijua kwamba kwa sasa dunia inakwenda kidijitali. Hivyo tujikite kuwekeza kwenye mifumo ambayo inamwezesha mwanafunzi kusoma akiwa popote badala ya kuendelea kujikita kwenye majengo ya maktaba,” amesema.
Akijibu hoja za wawakilishi hao wakati akihitimisha mjadala, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa, amesema Serikali inaendelea kufanya mabadiliko makubwa katika sekta hiyo, na ndio maana imetengewa bajeti kubwa kutokana na kipaumbele inachokitoa katika sekta hiyo.
Amesema imeshafanya mabadiliko mbalimbali ya mitalaa katika elimu ya kawaida na elimu ya amali.
