
Dodoma. Waziri MKuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Serikali inapanga kufanya maboresho katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima, hususan gharama na usumbufu wa kufuata huduma za maghala yaliyo mbali na maeneo yao ya uzalishaji.
Amesema hayo leo, Jumamosi, Mei 16, 2026, alipozungumza na wananchi wa Kata ya Mnenia, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, katika mwendelezo wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Amesema amesema Serikali imepokea malalamiko mbalimbali kuhusu utekelezaji wa mfumo huo, na kwamba hatua zinaendelea kuchukuliwa, ili kuhakikisha mfumo huo unawanufaisha wakulima kama ilivyokusudiwa.
“Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ni wananchi wasiyafuate maghala, maghala yawafuate wananchi pale walipo,” amesema.
Aidha, Dk Mwigulu amesema ataitisha kikao maalumu kitakachowahusisha wakuu wa mikoa pamoja na sekta zinazohusika kutoka maeneo yanayozalisha mazao yanayotumia mfumo wa stakabadhi ghalani, ili kufanya tathmini ya changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua.
“Nitaitisha kikao cha wakuu wa mikoa ya maeneo haya yanayozalisha mazao ambayo wananchi wake wamekuwa wakipata changamoto, ili tupate mpango kazi wa namna ya kumaliza tatizo hili,” amesema.
Ametaja baadhi ya mikoa inayohusika kuwa ni Dodoma, Singida, Simiyu, Tabora, pamoja na baadhi ya mikoa ya kusini inayozalisha mazao ya biashara, ikiwemo ufuta na dengu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeelekeza wanunuzi wa mazao kutumia taasisi za kifedha kupata mikopo badala ya kuwakopesha wakulima kabla ya mauzo ya mazao yao.
“Wenzetu wanaokwenda kununua haya mazao wasiwakope wakulima, wao wakakope benki. Benki ndiyo taasisi zinazotoa mikopo,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mfumo huo ili kuhakikisha wakulima wanapata huduma kwa urahisi na kunufaika ipasavyo na mazao yao.
