WHO yaainisha mlipuko wa Ebola Congo DR na Uganda kama dharura ya afya ya ummaWHO yaainisha mlipuko wa Ebola Congo DR na Uganda kama dharura ya afya ya umma

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeainisha mlipuko wa virusi vya Ebola vya Bundibugyo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda kama dharura ya afya ya umma inayotia wasiwasi kimataifa.

Limeeleza kwamba hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa sehemu ya pili ya Kifungu cha 12 kuhusu uamuzi wa dharura ya afya ya umma inayotia wasiwasi kimataifa, ikiwa ni pamoja na dharura za janga, kulingana na Kanuni za Afya za Kimataifa za 2005.

WHO imesema kwa msingi huo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Tedros Adhanom Ghebreyesus, baada ya kushauriana na nchi wanachama zinazokabiliwa na hali hiyo, ameamua kwamba aina ya Bundibugyo ya virusi vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda ni dharura ya afya ya umma inayotia wasiwasi kimataifa.

Hata hivyo, shirika hilo limesema kwamba kuenea kwa ugonjwa huo hakufikii kiwango cha “dharura ya janga” kulingana na ufafanuzi wa Kanuni za Afya za Kimataifa.

Kuhusu takwimu za hivi karibuni, WHO imesema kwamba kufikia Mei 16, 2026, kulikuwa na visa 8 vilivyothibitishwa kimaabara, visa 246 vinavyoshukiwa, na vifo 80 vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola katika jimbo la Ituri la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, visa viwili vimethibitishwa kimaabara, ikiwa ni pamoja na kifo cha mtu mmoja, ndani ya saa 24 mnamo Mei 15 na 16, 2026, kwa watu waliowasili nchini humo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

WHO imesema kwamba kuna hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu idadi halisi ya watu walioambukizwa na wigo wa kijiografia wa mlipuko huo, pamoja na uelewa mdogo wa uhusiano wa epidemiolojia kati ya visa vinavyojulikana na vinavyoshukiwa.

Awali, Waziri wa Afya wa Kongo, Samuel Roger Kamba Mulamba alikuwa amesema kwamba aina mpya ya virusi vya Ebola vinavyoenea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni “vikali sana na hakuna chanjo au matibabu maalumu ya kuvidhibiti.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *