
Felicien Kabuga, aliyekuwa ameshtakiwa kwa kufadhili mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda, jana Jumamosi alifariki dunia katika hospitali huko The Hague, nchini Uholanzi akiwa na umri wa miaka 91.
Iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) mwezi Aprili 2013 ilitoa waranti wa kukamatwa Kabuga.
Kabuga alitiwa mbaroni nchini Ufaransa mwezi Mei 2020 na kuhamishiwa katika tawi la Hague mwezi Oktoba mwaka huo. Kesi yake ilianza kusikiliza Septemba mwaka 2022.
Hata hivyo Septemba mwaka 2023, Chumba cha Mashauri cha Mahakama ya The Hague kilitoa uamuzi na kusitisha shauri hilo kwa muda usiojulikana mwezi mmoja baada ya Kabuga kuonekana kutokuwa na hali nzuri kiafya.
Baada ya hapo, mahakama iliagiza aendelee kuzuiliwa katika kitengo cha Umoja wa Mataifa akisubiri uamuzi wa kuachiwa huru kwa muda.
Alizaliwa mwaka wa 1935 katika mkoa wa Byumba kaskazini mwa Rwanda, ambao sasa unajulikana kama wilaya ya Gicumbi karibu na mpaka wa Uganda. Kabuga aliibuka kutoka mtu wa kawaida na kuwa mmoja wa wafanyabiashara tajiri zaidi wa Rwanda.
Alituhumiwa kwa kutumia utajiri wake kufadhili mauaji ya kimbari ya mwaka nchini Rwanda 1994 dhidi ya kabila la Watutsi, ambapo karibu Watutsi milioni 1 na Wahutu wenye misimamo ya wastani waliuawa katika muda wa siku 100.
