
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) Mohammad Baqir Qalibaf amesema kuwa muqawama wa kishujaa wa taifa la Iran kwa muda wa siku 70 umekuwa msukumo katika kuharakisha mageuzi ambayo hayajaonekana katika karne moja, na hivyo kuashiria mapambazuko ya mfumo mpya wa kambi kadhaa.
“Ulimwengu unasimama kwenye kilele cha utaratibu mpya,” ameeleza Qalibaf sikuya Jumamosi.
Spika wa Bunge la Iran amemnukuu Rais Xi Jinping wa China na kusema kuwa “mabadiliko ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika karne hii yanaongezeka duniani kote,” na kuongeza: “Ninasisitiza kuwa muqawama na mapambano ya siku 70 ya taifa la Iran umeongeza kasi ya mabadiliko haya.”
Matamshi haya ya Qalibaf yanatilia mkazo mchango mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu kwa ulimwengu unaoibukia wa kambi nyingi. Kwa muda wa siku 70, taifa la Iran limesimama kidete kwa umoja, mshikamano na malengo ya mapinduzi, na kukwamisha njama za maadui, Marekani na Israel, na washirika wao wa kikanda.
Amesema, kuanzia Amerika Kusini hadi Afrika na Asia, nchi zinazoendelea duniani zimezidi kutambua kwamba zama za udhibiti wa Magharibi, zilizotawaliwa na vikwazo, hatua za kijeshi na udhibiti wa kiuchumi, zinakaribia mwisho.
Uzoefu wa Iran umethibitisha kuwa umoja, kujitegemea na kushikamana na Mhimili wa Muqawama kunaweza kuharakisha kuibuka mfumo wa kimataifa wa haki na usawa.
