
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) yenye makao yake The Hague imeripotiwa kutoa hati tano za “siri” za kukamatwa kwa maafisa wa utawala wa Israel, wakiwemo wanasiasa watatu na maafisa wawili wa kijeshi.
Vyombo vya habari vimeripoti Jumapili kwamba haijabainika wazi ni lini hati hizo zilitolewa. ICC imekuwa na utaratibu wa kutoa baadhi ya hati zake za kukamatwa kwa siri na baadaye kuzitangaza hadharani.
Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na ICC kuhusu ripoti hiyo. Endapo itathibitishwa, idadi ya maafisa wa Israel wanaokabiliwa na hati za kukamatwa na mahakama hiyo itafikia saba.
Mahakama hiyo ya The Hague tayari ilitoa hati za kukamatwa mnamo Novemba 2024 dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa vita Yoav Gallant, kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, kufuatia vita vilivyoanzishwa dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza Oktoba 2023.
Tangu wakati huo, majeshi ya Israel yameripotiwa kuua zaidi ya watu 72,000 katika eneo hilo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi zaidi ya 172,000.
Utawala wa Tel Aviv umekuwa ukitoa vitisho na onyo dhidi ya ICC kufuatia kuanzishwa kwa uchunguzi wa uhalifu wa kivita unaohusishwa na Israel huko Gaza.
Ripoti iliyochapishwa na jarida la Middle East Eye (MEE) mwezi Agosti 2025 ilifichua kwamba Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Karim Khan kutoka Uingereza, aliambiwa afute hati za kukamatwa dhidi ya maafisa wa Israel, vinginevyo yeye binafsi pamoja na ICC “wangeangamizwa.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, onyo hilo liliwasilishwa mwezi Mei kwa Khan na Nicholas Kaufman, mwakilishi wa kijeshi mwenye uraia wa Uingereza-na Israel ambaye anashikana na Netanyahu.
