Geita. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche amesema jaribio lolote la kutaka kukifuta chama hicho halitafanikiwa kwa kuwa wananchi wana imani nacho na kuongeza kuwa hawako tayari kuona kikifutwa.
Licha ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukiandikia chama hicho kutaka kijieleze kwa nini kisisimamishwe usajili, kiongozi huyo amesema hawatishiki na barua hiyo huku akidai ina lengo la kukinyamazisha dhidi ya ajenda ya kudai Katiba mpya.
Katika barua ya Msajili ya Mei 7, 2026, iliyoelekezwa kwa katibu Mkuu wa Chadema, ikisainiwa na Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza, ilikielekeza chama hicho kujieleza kwa nini kisisimamishiwe usajili wake kutokana na matamshi ya viongozi wake ambayo amedai ni ya kichochezi.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, juzi, Nyahoza alifafanua kwamba barua ya Msajili inaeleza wazi adhabu ya makosa hayo kuwa ni kusimamishiwa usajili, kulipa faini au vyote kwa pamoja, endapo hataridhika na maelezo yao kuhusu makosa waliyoyafanya.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Satellite uliopo mamlaka ya mji mdogo wa Katoro, mkoani Geita.
Heche alizungumza hayo Mei 16, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Satellite uliopo mamlaka ya mji mdogo wa Katoro, mkoani Geita, ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya Chadema yenye dhima ya kudai Katiba mpya pamoja na kuachiwa kwa mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa kamati kuu wa Chadema, viongozi wa mikoa na wilaya na wanachama wa chama hicho kutoka maeneo mbalimbali mkoani humo.
Heche amesema licha ya kuwepo kwa taarifa kuhusu yeye kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini, hana mpango wa kutoroka, akiamini kuwa ana wajibu wa kuwatetea wananchi na misingi bora ya utawala wa kidemokrasia nchini.
“Sitakimbia nchi yangu kwa sababu mimi ninaamini katika demokrasia, mpira uwekwe mezani na mimi nawaomba wananchi nguvu yetu ni nyie, kama tusingekuwa na nyie pengine ningeambiwa nikimbie,” amesema.
Aidha, Heche ameiomba jamii kuungana na chama hicho bila kujali itikadi na imani zao katika kukemea vitendo vya utekaji nchini ambavyo vimekuwa vikiathiri ustawi wa wananchi.
Amesema msimamo wa Chadema utaendelea na kutoitambua ripoti ya Jaji Chande iliyokuwa ikichunguza vurugu za wakati na baada ya uchaguzi. Licha ya kutoitambua ripoti hiyo, chama hicho kimetaka ripoti hiyo kuwekwa wazi ili isomwe na kuchambuliwa na wananchi wote kwa kuwa inagusa maisha yao na ndugu zao waliofariki kwenye vurugu wakati wa uchaguzi.
“Tunataka iwekwe hadharani, wananchi waichambue, wajue kilichomo,” ameongeza Heche wakati akizungumza kwenye mkutano huo.
Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema barua iliyotumwa na Msajili wa Vyama vya Siasa akitaka chama hicho kijieleze kwa nini kisipigwe faini au kusimamishiwa usajili, ni hila zinazofanywa na msajili dhidi yao baada ya kutangaza msimamo wa kamati kuu wa kutoitambua ripoti ya Jaji Chande.
Pia, amesema lengo la barua ya msajili ni kutaka kuwapotezea lengo la kujadili umuhimu wa kupatikana kwa Katiba mpya.
Kuhusu mashtaka dhidi ya mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuyaenzi mambo aliyokuwa akiyapigania ikiwa ni pamoja na madai ya Katiba mpya.
Mnyika ametaja njia mbili zinazoweza kumfanya Lissu kuachiliwa huru bila dhamana ikiwa ni siku zaidi ya 400 tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025 huko Mbinga mkoani Ruvuma.
Amezitaja njia hizo kuwa ni Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini na Mwendesha Mashtaka Mkuu (DPP), kuwasilisha mahakamani hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka yanayomkabili Lissu kwa kuwa hayana masilahi kwa umma.
Pili Mahakama inatakiwa kutumia wajibu wake wa kikatiba kutoa haki ya kusikilizwa kwa wakati kwani tangu Februari 24, 2026, Lissu hajafikishwa mahakamani bila sababu za msingi.
Mnyika amesema endapo njia hizo hazitafanikiwa, watatumia njia mbadala kushinikiza aachiwe huru bila kuathiri Katiba na mamlaka za kimahakama ikiwa ni pamoja na kufanya maombi kila mtu kwa imani yake pamoja na kufanya maandamano huru.
Naye, mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, Godbless Lema ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya uchumi, ametoa rai kwa wananchi kuchangia chama hicho ili kifanye shughuli za kisiasa.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Satellite uliopo mamlaka ya mji mdogo wa Katoro, mkoani Geita.
Pia, amewataka wafanyabiashara ikiwa watahofia kufanya siasa za jukwaani kushiriki kwa kuchangia kupitia Tone tone ili wakatetee masilahi yao.
“Wananchi milioni moja wakijiandikisha katika mchango wa kujirudia, mtakuwa mnatupa Sh1 bilioni kila mwezi, mkiwa 500, Sh500 milioni kila mwezi, hatari ya nyie kutochangia chama chenu, mtaua vipaji vyenye uwezo kuliko sisi kwa sababu hawawezi kutembea bila kuwezeshwa,” amesema Lema.
