
Dar es Salaam. Katika tukio la kustaajabisha samaki aina ya papa mwenye urefu wa mita nne amemvamia na kumshambulia mwanaume ambaye bado hajatambuliwa jina lake, na kusababisha kifo chake nchini Australia.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 38 ameuliwa na papa huyo mkubwa na hatari zaidi duniani aina ya ‘Great White’ huko pwani ya kisiwa cha Rottnest maarufu kwa utalii, kuogelea na mchezo wa kuteleza juu ya mawimbi, hivyo inawezekana alikuwa akijihusisha na shughuli za baharini, lakini taarifa rasmi kuhusu shughuli aliyokuwa akifanya bado hazijatolewa.
Tukio hilo limetokea jana Jumamosi Mei 16, 2026, ambapo video zilizochukuliwa eneo la tukio zikionyesha mtu huyo akiletwa ufukweni kwa kutumia boti, huku wahudumu wa afya na polisi wakifanya juhudi za kumuokoa.
Vyombo vya habari vya Australia vilivyonukuliwa na BBC pamoja na DW vimeeleza kuwa kutokana na majeraha ya kung’atwa na papa huyo majeruhi alifariki dunia. Aidha shambulio hilo linatajwa kuwa la kwanza la papa kusababisha kifo nchini humo tangu Machi mwaka jana, wakati mvuvi aliposhambuliwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa tangu mwaka 1791, Australia imerekodi mashambulizi karibu 1,300 ya papa, huku zaidi ya watu 260 wakifariki dunia.
Wataalamu wanaamini ongezeko la joto baharini na shughuli nyingi za binadamu majini vinaweza kubadili mienendo ya papa na kuongeza mashambulizi.
