
Moshi. Wakati Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC, ikiona wagonjwa wa saratani takribani 6,000 kila mwaka, asilimia 40 ya wagonjwa hao ambao wanahitaji tiba ya mionzi ni watoto.
Hayo yamesemwa leo Mei 17, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Gileard Masenga wakati wa matembezi ya hisani ya kuchangia mahitaji ya watoto wenye saratani wanaotibiwa katika hospitali hiyo, yaliyoandaliwa na wa Waokaji Tanzania (Bakers Meetup Tz).
“Hapa KCMC tunaona wagonjwa wengi wa saratani kwa mwaka, wagonjwa wanaoonwa wanaweza kufikia hadi 6,000 kwa mwaka. Lakini wagonjwa wapya wanaweza kufika 1,500,” amesema Profesa Masenga.
Profesa Masenga amesema kwa sasa hospitali hiyo inatoa tiba kamili ya saratani na kwamba imekuwa na mafanikio makubwa zaidi kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kupata matibabu.
“Kama mnavyofahamu, saratani inatibika kwa mionzi, asilimia 60 ya wagonjwa wa saratani wanahitaji tiba ya mionzi hapa KCMC miongoni mwao asilimia 40 ni watoto. Sasa hivi haihitajiki tena kuwatuma wagonjwa wa saratani kwenda Ocean Road.
“Kutoa tiba kamili hapa KCMC imekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wanaoishi kanda hii ya Kaskazini,” amesema Profesa Masenga.
Amesema: “Tuliamua kwenda kwa watoto kwa sababu tuliona kwamba saratani nyingi za watoto zinapona lakini watapona wakija mapema na kupata tiba kamili, na tiba kamili inachukua muda, kuna watoto pale wamekaa hadi miaka miwili lakini wengi ni miezi sita hadi mwaka mmoja.”
Profesa Masenga amesema saratani ambayo imekuwa ikiwasumbua watoto wengi ni ya damu ambayo amesema matibabu yake yakiwahiwa inapona.
“Watoto wengi ambao tunawaona hapa ni wenye saratani ya damu (leukemia), macho na tezi lakini nyingi zinapona zikiwahiwa. Changamoto tunayoipata ni kwamba wengi wanakuja wakiwa wamechelewa kwa sababu ya utambuzi.
“Utambuzi umekuwa ni changamoto katika hatua ya familia na hospitali nyingi hizi za kati kwa sababu mtoto anaweza kuwa na homa isiyopona kumbe ana saratani,” amesema Profesa Masenga.
Profesa Masenga amesema tangu kuanza kutolewa kwa huduma ya tiba ya mionzi hospitalini hapo mwaka huu, watoto 80 wamefanikiwa kupata matibabu hayo.
Akizungumza na daktari bingwa wa magonjwa ya damu na saratani za watoto wa hospitali hiyo, Dk Ester Majaliwa amesema saratani si laana wala uchawi, bali ni ugonjwa ambao unaweza kuwatokea watoto na ukigundulika mapema unatibika kabisa.
Aidha, amewataka wazazi kuwa makini na kufuatilia mabadiliko ya afya za watoto wao, hasa wanapougua mara kwa mara bila kupona licha ya kupatiwa matibabu.
Ametaja baadhi ya dalili zinazopaswa kupewa uzito kuwa ni pamoja na mtoto kupungua uzito, kutapika mara kwa mara, kuchoka kupita kiasi na homa zisizoisha licha ya kutumia dawa.
“Mtoto anapoanza kuumwa na haponi ndani ya wiki ya kwanza au ya pili baada ya kupatiwa matibabu, wazazi wasichukulie hali hiyo kuwa ya kawaida, inaweza kuwa ni dalili ya saratani, hivyo ni muhimu mtoto kufanyiwa vipimo zaidi,” amesema Dk Majaliwa.
Akizungumza na mmoja wa wadau wa hospitali hiyo, Yuvenal Shirima ameihimiza jamii kushirikiana kwa pamoja kuwasaidia watoto wenye changamoto ya saratani, akieleza kuwa mahitaji yao ni makubwa na yanahitaji msaada wa wadau.
“Kama mdau, nimeona ni muhimu kuwa sehemu ya juhudi hizi kwa sababu wazazi wa watoto wetu wenye changamoto ya saratani wanapitia hali ngumu sana, hivyo jamii inapaswa kushirikiana na hospitali kuwasaidia watoto hawa, kwani wanahitaji mahitaji mbalimbali,” amesema Shirima.
